MRADI WA TAZA KUUNGANISHA UMEME AFRIKA.

MUUNGANO   MEDIA
0


Dkt. Biteko aweka Jiwe la Msingi

Aitaka TANESCO Kusimamia Mradi kikamilifu

Ataka Wakandarasi wazembe Wachukuliwe Hatua

TAZA kuiwezesha Rukwa kupata umeme wa gridi


Serikali imesema kuwa mradi mkubwa wa usafirishaji umeme wa TAZA

unaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti

400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga na kuunganisha Tanzania na Zambia

(TAZA) pamoja na vituo vya kupoza umeme vya Tagamenda, Kisada, Iganjo,

Nkengamo na Malangali utawezesha kuunganisha Bara la Afrika kwa

nishati ya umeme kutoka Afrika Kusini hadi Ethiopia.


Hayo yameelezwa leo Julai 29, 2024 Sumbawanga mkoani Rukwa na

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati

akiweka jiwe la msingi la utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa

usafirishaji umeme ambao unahusisha


kipande cha kilomita 4 kutoka Tunduma hadi Nakonde mpakani mwa

Tanzania na Zambia.


“ Kwa kutambua kuwa nishati ni kichocheo cha uchumi, Serikali

imeendelea kutekekeza miradi mbalimbali ukiwemo wa Julius Nyerere

(JNHPP) ambao tayari unaingiza megawati 705 kwenye gridi ya Taifa na

hivyo kuwezesha nchi kuwa na ziada ya umeme huku mtambo mwingine wa

megawati 235 ukitarajiwa kuwashwa mwezi Agosti”, amesema Dkt. Biteko


Ametaja miradi mingine inayotekelezwa kuwa ni wa umeme Jua wa Kishapu

(MW 150), Malagarasi (MW 49.5) na ya Gesi Asilia huku lengo likiwa ni

kuwa na uhakika wa umeme wa kutosha.


Pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo, Dkt. Biteko amesema uzalishaji

wa umeme lazima uende pamoja na kazi ya uungashiaji umeme wananchi

kupitia miradi mbalimbali kama wa TAZA ambao unawahakikishia Wanarukwa

upatikanaji wa umeme wa gridi ambao utakuwa wa uhakika na wa kutosha.


Amesema kwa sasa Mkoa wa Rukwa unapata umeme kwa kiasi kikubwa kutoka

nchini Zambia kwa gharama ya shilingi bilioni 15 kwa mwaka hivyo

kukamilika kwa mradi huo kutaifanya Tanzania kuacha kununua umeme

kutoka nchi hiyo isipokuwa nyakati za dharura.


Ameongeza kuwa, mradi wa TAZA utafaidisha pia maeneo yanayopitiwa na

mkuza kutoka mkoani Iringa hadi Rukwa kupitia vituo vya kupoza na

kusambaza umeme na kuwezesha kufanyika kwa biashara ya umeme katika

nchi zilizopo Mashariki mwa Afrika kupitia Southern African Power

Pool (SAPP) na Easten Africa Power Pool (EAPP).


Kuhusu usimamizi wa mradi huo, Dkt, Biteko pamoja na kuipongeza

TANESCO kwa utendaji mzuri wa kazi, ameiagiza taasisi hiyo kuhakikisha

kuwa kasi ya utekelezaji mradi wa TAZA inaendelea kuwa kubwa, na

kwamba tukio la kuwekwa kwa jiwe la msingi lisiishie kwenye kupiga

picha na kisha kutokomea bali wausimamie mradi huo ili ulete matokeo

tarajiwa.


Akigusia usambazaji wa umeme vijijini mkoani Rukwa, Dkt.Biteko amesema

kuwa Serikali haifurahishwi na kasi yake ya utekelezaji wa miradi

kwani analalamikiwa kusuasua na hivyo ameagiza kuwa ifikapo Agosti

mwaka huu awe amemaliza kazi na asipotekeleza agizo hilo achukuliwe

hatua za kimkataba na hii inajumusha pia wakandarasi wengine wazembe

ikiwemo katika Mkoa wa Kagera.


“Kazi za umeme vijijini zinaombwa na kampuni za nje ya nchi na

kampuni za ndani, tunaonekana wabaya kwa kuzibana sana kampuni za nje

lakini za ndani tunabembelezana, Katibu Mkuu na DG REA nataka nione

hatua zinachukuliwa, haiwezekani wakandarasi wageni tunawabana halafu

wa ndani wanaharibu miradit, wananchi wanalalamika halafu

tunabembelezana, hii hapana.” Amesisitiza Dkt. Biteko


Amesema Serikali inataka kumaliza kazi ya usambazaji umeme vijijini na

kuhamia vitongojini na kwamba lengo ni kuwa ifikapo mwezi wa 12 mwaka

huu vijiji vyote viwe vimesambaziwa umeme.


Kuhusu utekelezaji wa TAZA, Dkt. Biteko ameshukuru Wafadhili wa mradi

huo ambao ni Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Ufaransa

(AFD), Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) ambao kwa pamoja wametoa zaidi ya

shilingi Trilioni Moja za kutekeleza mradi huo ambao pia unahusisha

ujenzi wa vituo vitano vya kupiza umeme. Amesema Serikali ya Awamu ya

Sita inawajali wafadhili wetu.


Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali

itaendelea kuipa kipaumbele ajenda husika kwani imeshaanzisha Kitengo

cha kushughulikia nishati hiyo ndani ya Wizara na kwamba Benki ya

Dunia imeahidi kuangalia namna ya kuiwezesha Serikali kutekeleza

ajenda hiyo.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere amesema mradi wa TAZA

utaihakikishia Rukwa umeme wa uhakika, pia kuimarisha uwekezaji ambapo

amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji

wa miradi ya umeme vijijini ambapo tayari vijiji 308 vina umeme huku

31 vilivyobaki kazi ikiendelea.


Kwa upande wake, Katibu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi

Mramba amesema mradi wa TAZA ni wa kipekee kwa sababu utawezesha

Afrika kuunganishwa na umeme kutoka Afrika Kusini hadi Ethiopia.


Naye, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Mathew

Mkingule ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa

utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa umeme wa TAZA ambao amesema utahakikisha usalama wa nishati katika nchi za Kusini mwa Afrika, kukuza uchumi Mkoa wa Rukwa, kuwezesha biashara ya umeme, fursa ya ajira na kulinda mazingira kwani nishati ya umeme inawezesha wananchi kutumia nishati hiyo katika kupikia.


Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete kwa niaba ya

Wawekezaji wa mradi amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa

Nishati, Dkt. Doto Biteko pamoja na Serikali kwa ujumla kwa miongozo

ambayo imewezesha mradi wa TAZA kuanza kutekelezwa.


Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga

alieleza kuwa, mradi wa TAZA ni sehemu ya maazimio ya yaliyofanyika

tarehe 15 Desemba 2014 baina ya Tanzania, Kenya na Zambia ya

kuunganisha gridi za nchi hizo tatu.


Katika utekelezaji wa makubaliano hayo, amesema Tanzania ilianza

kujenga laini ya umeme ya kV 400 ya km 670 kutoka Dodoma hadi

Shinyanga ambayo ilishakamilika na baadaye kujenga laini ya kV 400

kutoka Singida hadi Namanga kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya ambao

umekamilika kwa asilimia 99.8 na kipande cha tatu ni cha mradi wa

TAZA ambacho kinatekelezwa sasa ili kuunganisha gridi ya Tanzania na

Zambia.


Amesema mradi umeshaanza na umefikia asilimia 29.8 huku ukitarajiwa

kukamilika Mei 2026.


Wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ni Naibu Katibu MKuu

Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, Wenyeviti na Makamu Wenyeviti

wa kamati mbalimbali za Bunge ikiwemo ya Bajeti, Hesabu za Serikali,

Nishati na Madini, Mwakilishi wa AU, na AFD, Katibu Mtendaji wa EAPP,

Bodi na Wakurugenzi wa Taasisi chini ya Wizara, Menejimenti Wizara ya

Nishati pamoja na Watendaji kutoka Shirika la Umeme la Zambia (ZESCO).


Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)