Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe amewaongoza wajumbe wa timu ya Menejimenti ya Idara ya Kinga kutembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa jengo la Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma lililopo katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma.
Aidha Dkt. Kapologwe ameridhishwa na hatua ya ujenzi wa jengo hilo ilipofikiwa na kuwataka viongozi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kuongeza kasi katika usimamizi ili jengo hilo liweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutumika kama ilivyokusudiwa
''Hadi sasa hatua iliyofikiwa ni nzuri kwa hiyo niombe muongeze kasi ya usimamizi ili shughuli za umaliziaji zikamilike na hata nikiangalia ni vitu vichache vimebaki vya kumalizia kwa hiyo mjitahidi ili hadi kufikia mwezi Septemba, 2024 jengo hili lianze kufanya kazi iliyokusudiwa " amesema Dkt. Kapologwe.
Katika hatua nyingine Dkt. Kapologwe ametoa wito kwa watumishi na Viongozi wa Idara ya Kinga kuweza kufanya kazi kwa pamoja na kwa kushirikiana bila kujali vitengo wanavyofanyia kazi ili kila mmoja kujua majukumu na utendaji kazi wa Idara kwa ujumla
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Dkt. Tumaini Haonga amesema kuwa jengo hilo litakapokamilika litawezesha shughuli mbalimbali za Wizara ya Afya kufanyika hapo ikiwemo huduma za uchapaji wa vitabu na Miongozo mbalimbali ya Wizara ya Afya, Kituo cha huduma kwa wateja (Afya Call Center ), Studio kwa ajili ya matangazo na vipindi vya Uelimishaji umma kuhusu masuala mbalimbali ya Afya pamoja na ukumbi za mikutano.
Jengo hilo jumuishi la Elimu ya Afya kwa Umma ambalo ujenzi wake ulianza mwaka 2022 linatarajia kukamilika hivi karibuni na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa