Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale
amesema Wakuu wa Wilaya wanapatiwa mafunzo na Ofisi ya Rais -
TAMISEMI ya kuwajengea uwezo wa kusimamia zoezi la utoaji na
urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri za Wilaya
kwa akina mama, vijana na wenye ulemavu.
Bw. Mtwale amesema hayo leo katika Ukumbi wa Shule ya Uongozi ya
Mwalimu Julius Nyerere Kibaha mkoani Pwani kwa Niaba ya Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bw. Adolf Ndunguru wakati akifungua kikao kazi
cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa
na Wakuu wa Wilaya zote nchini.
Bw. Mtwale amesema, Serikali imeanza kutoa mikopo ya asilimia 10 baada
ya hapo awali kusitishwa kutokana na changamoto jilizojitokeza, na
kuongeza kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeshapitia kanuni na kufanya
maboresho na ikaona ni vema Wakuu wa Wilaya wakapitishwa katika
kanuni hizo ili waweze kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa utoaji wa
mikopo hiyo.
“Tumeona ni vema nanyi mkapitishwa katika kanuni hizo ili tuwe na uelewa
wa pamoja katika kusimamia utoaji wa mikopo hiyo ili mikopo hiyo iwe na
tija kwa watakaonufaika na katika taifa kwa ujumla,” Bw. Mtwale
amesisitiza.
Sanjali na hilo, Bw. Mtwale amesema Wakuu wa Wilaya watapitishwa
katika taarifa ya ukaguzi ya mwaka wa fedha 2022/23 ili wafahamu hoja
zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwani
nao ni wasimamizi wa halmashauri zilizopo katika maeneo yao ya utawala.
Ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wakuu wa Wilaya
nchini, Bw. Mtwale amesema Ofisi ya Rais - TAMISEMI imemualika
mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt.
Garvin Kweka ili kuwapatia elimu ya afya ya akili na ya namna bora ya
kuepukana na magonjwa ya afya ya akili.
Akiwasilisha mada kuhusiana na afya ya akili, mtaalamu wa afya ya akili
kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Garvin Kweka amewataka
Wakuu wa Wilaya kuzingatia mahusiano ya kijamii ili kujenga afya nzuri ya
akili itakayowawezesha kutekeleza kikamilifu majukumu yao kwa ufanisi.
“Mtu anayeenda kwenye jumuiya, vikoba, kanisani au msikitini akipata
msiba, msiba wake hauwi sawa na mtu anayejifungia ndani hivyo
mahusiano ya kijamii ni lazima yazingatiwe na kisingi ndio utulivu wa afya
ya akili,” Dkt. Kweka amesisitiza.
Kikao kazi hicho cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe.
Mohamed Mchengerwa na Wakuu wa Wilaya zote nchini, chenye lengo la
kuwajengea uwezo kiutendaji viongozi hao kinafanyika kwa siku mbili
katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani
Pwani.