Askari wa Jeshi la Polisi Mkoani
Songwe wametakiwa kutambua kuwa kazi ya Polisi ni kazi takatifu ambayo
majukumu yake yanahusiana na makatazo na amri za Mungu.
Kauli
hiyo imetolewa Mei 22, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Agustino Senga alipofanya baraza na
Maafisa, Wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali.
“Makatazo
yaliyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu yana mahusiano makubwa na kazi ya
Polisi hasa katika amri za Mungu ambazo katika nyumba za ibada
wanaziita dhambi huku kwetu ni uhalifu inatupasa kuzuia vitendo hivyo
ili jamii iwe salama” Kamanda Senga alisema hayo
Kamanda Senga
alisema watendaji wa Jeshi la Polisi ni kioo kwa jamii hivyo basi
wanapaswa kuendelea kulinda taswira nzuri ya Jeshi la Polisi kwa Jamii
kwa kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili
jamii iendelee kukimbilia na kushirikiana nalo katika kutoa taarifa za
wahalifu na uhalifu.
Naye, Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa
Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Gallus Hyera aliwasisitiza askari
kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia wimbo wa maadili na kauli mbiu ya
Jeshi la Polisi ambayo inawataka kufanya kazi kwa nidhamu, haki, weledi
na uadilifu.