Serikali imeanza kufanya marekebisho ya kubadili muundo wa Baraza la
Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kuwa Mamlaka
ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA).
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Khamis Hamza Khamis amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa
Viti Maalumu Mhe. Maryam Azan Mwinyi aliyetaka kujua ni lini Serikali
itawasilisha Marekebisho ya Sheria ya Mazingira ili kuipa NEMC uwezo
wa hadhi ya Mamlaka.
Amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kuwa hadi
kufikia Juni 2024, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa
Mazingira Sura 191 uwasilishwe katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa hatua zaidi.
Akiendelea kujibu swali hilo Naibu Waziri Khamis amesema kuwa
marekebisho hayo ya kubadili muundo huo ni moja ya
masuala yanayopendekezwa kufanyiwa marekebisho ili NEMC iwe
Mamlaka.
Akiendelea kujibu maswali ya nyongeza ya mbunge huyo, Mhe. Khamis
amesema kuwa miongoni mwa majukumu ya mameneja wa kanda wa
NEMC ni kusimamia sheria pamoja na kutoa elimu kwa jamii.
Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza kwa utendaji kazi mzuri na kusema
kuwa majukumu hayo yanaweza kufanyiwa marekebisho kulingana na
sheria itakavypendekeza.
Hivyo, Naibu Waziri Khamis amesema kuwa NEMC itakayofahamika kama
NEMA itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na Mamlaka ya Usimamizi wa
Mazingira (ZEMA) katika utekelekezaji wa majukumu ili usimamizi wa
mazingira nchini uwe endelevu na wenye mafanikio.