Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo ameendelea kuhimiza matumizi ya nishati safi ya
kupikia ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa
miti.
Ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na Shirika la Utangazaji la
Zanzibar (ZBC) wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
2024 katika Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro
uliofanywa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Aprili 02, 2024.
Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali ilitangaza kusitisha matumizi ya kuni na
mkaa kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuanzia Januari 2024
ambapo tayari taasisi hizo zimetekeleza maelekezo hayo.
Amesema kuwa kila mwaka takriban hekta laki nne za misitu zinapotea
kutokana na kukatwa kwa ajili ya kuni na mkaa hivyo Serikali
inahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuinusuru.
“Utunzaji wa mazingira unagusa mambo mengi, hivi karibuni Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan alizindua Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuhifadhi
mazingira,“ amesisitiza.
Aidha, Waziri Jafo amesema kuwa Mwenge wa Uhuru mwaka huu
umeleta faraja kubwa katika utunzaji wa mazingira kwani utakimbizwa
mikoa yote hivyo utasaidia wananchi kuelewa dhana nzima ya utunzaji
wa mazingira na changamoto kubwa kwa sasa ni utunzaji wa mazingira
Itakumbukwa kuwa katika kilele cha Mwenge wa Uhuru 2023
kilichofanyika Oktoba 14 mkoani Manyara, Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alitoa rai kwa Ofisi
ya Waziri Mkuu kuendelea kutumia ujumbe unaohamasisha jamii utunzaji
wa mazingira ili kusaidia kulinda na kutunza Mazingira.
Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 una kaulimbiu "Tunza Mazingira na
Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelezu"
ambayo inaweka msisitizo kwa namna nyingine katika uhifadhi wa
mazingira.