Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa Wakuu wa Taasisi Wanawake, kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwekeza kwa Wanawake na kuharakisha maendeleo ya mwanamke kwa Taifa.
Waziri Dkt. Gwajima amesema hayo wakati akizungumza na Wanawake Wakuu wa Taasisi, Mashirika na Vyuo vya Umma katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Machi 07, 2024 jijini Dar Es Salaam.
Amewahamasisha pia kuanzisha jitihada za programu mbalimbali za kuinua Wanawake nchini katika shughuli mbalimbali za Kiuchumi kwenye ngazi za Mamlaka wanazozisimamia ili kusaidia kundi kubwa la watu na kuendeleza Taifa poja na kuratibu wanawake viongozi wote kuwa na Jukwaa kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kuwawezesha wanawake wanaoanza safari ya uongozi
'Ni ukweli usiopingika kuwa, kwa namna tunavyoshuhudia Wanawake wapambanaji nchini kwetu, katika shughuli mbalimbali za biashara na uchumi, tunatamani siku moja tuwaone miongoni mwa watu waliofanikiwa sana katika uchumi hapa nchini kwetu na duniani kwa ujumla. Naamini hili linawezekana." amesisitiza Dkt. Gwajima.
Katika kuendeleza jitihada hizo, Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali ya Rais Samia, imeendelea kuinua Wanawake katika nafasi mbalimbali za kimaamuzi na uongozi ambapo wameonesha umahiri katia nafasi hizo.
Aidha, Waziri Dkt. Gwajima ameelezea Programu ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kuhusu Jukwaa la Kizazi chenye Usawa inavyotekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo kuongeza kazi zenye staha kwa kuendeleza biashara na urasimishaji wa biashara za wanawake na kuboresha upatikanaji na matumizi ya teknolojia nafuu na zinazofaa ili kuongeza uwezo wa wanawake wa kuzalisha bidhaa zenye ushindani wa soko la ndani na nje.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Latifa Khamis amesema, nguvu ya wanawake inajengwa na umoja na kushirikiana hivyo amewaasa wanawake nchini kuungana na kupeana moyo katika sbughuli zao. Aidha amemshukuru Waziri Dkt. Gwjima kwa kuwawezesha wanawake hao kuwa na umoja huo tangu mwaka 2021.
Maadhimisho hayo yamehudhuirwa na viongozi mbalimbali wanawake wakiwemo Kamishna wa uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala, Balozi mstaafu wa Tanzania nchini Marekani Mhe.Amina Salum Ali, Mtendaji Mkuu Mfuko wa mawasiliano kwa wote Justina Mashiba, Mtendaji Mkuu Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bengi M. Issa, Mkurugenzi Shirika la Taifa la Takwimu Dkt. Albina Chuwa na Mkuu wa Chuo cha DMI Dkt. Tumaini Gurumo.
MWISHO

