Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar (SMZ) zimefanikiwa kutatua hoja 21 za Muungano kati ya 25
zilizokuwepo awali.
Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani
Jafo amesema hayo katika Kikao cha Mawaziri wa SJMT na SMZ cha
kujadili Masuala ya Muungano kilichofanyika Nyamanzi, Zanzibar leo Machi 05,
2024
Amesema kuwa tangu mchakato wa kutatua changamoto hizo ulipoanza, hadi
sasa zimebaki hoja nne za Muungano ambazo Serikali zote mbili zinaendelea
kuzitafutia ufumbuzi.
Dkt. Jafo ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa kikao hicho amesema viongozi wa
pande zote mbili za Muungano wamekaa pamoja kujadili hoja hizo nne za
Muungano zilizobaki na kuangalia namna ya kuzipatia ufumbuzi.
Amezitaja hoja nne zilizobaki kuwa ni pamoja na Suala la Sukari, Usajili wa
Vyombo vya Moto, Bodi ya Pamoja na Mgawanyo wa Mapato ya iliyokuwa
Sarafu ya pamoja ya Afrika Mashariki.
Kutokana na mafanikio, Dk. Jafo amewapongeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa kazi
kubwa wanayoifanya katika kutatua hoja zilizobaki.
“Niwapongeze pia Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wataalamu mbalimbali
kutoka Serikali za pande zote za Muungano kwani wamefanya kazi kubwa ya
kuchakata changamoto zilizokuwepo hadi kufikia mafanikio haya,“ amesema
Dkt. Jafo.
Kwa upande Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili ya Rais (Sera, Uratibu na
Baraza la Wawakilishi) Mhe. Hamza Hassan Juma amesema kuwa lengo la
kikao hicho ni kuzungumzia hoja mbalimbali zinazokabili utendaji wa shughuli
za SJMT na SMZ.
Amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umedumu kwa muda
mrefu kutokana viongozi wa pande zote mbili za Muungano kukaa pamoja na
kujadili changamoto zinazojitokeza kwa uwazi na kuzipatia ufumbuzi kwa
pamoja.
Akitolea mfano wa mafanikio ya Muungano huu, Mhe. Hamza amesema
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayoundwa na nchi nane inaendelea
kudumu kutokana na uzoefu unaopatikana Tanzania na hivyo jumuiya hiyo
kuendelea kukua.
Ameongeza kuwa hoja nyingi zimeshatatuliwa hivyo mkutano huo unatoa
matumaini makubwa kupatikana kwa maslahi ya wananchi wa pande zote
mbili pamoja na kuendelea kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ambao unatimiza miaka 60 ifikapo Aprili 26, 2024.
.jpg)
