SERIKALI imewataka maafisa forodha na wasimamizi wa sheria mipakani kuendelea
kuimarisha usimamizi na udhibiti wa kemikali zinazodhibitiwa zinazochangia kumong’onyoa
tabaka la ozoni kunakochangia ongezeko la joto duniani na husababisha mabadiliko ya
tabianchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan
Mitawi katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira, Mhandisi
Catherine Bamwenzaki wakati akifungua Mafunzo ya Maofisa Forodha na Wasimamizi wa
Sheria mipakani kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya
Montreal leo Jumamosi Februari 17, 2023 katika ukumbi wa Mpaka wa Sirari, Mkoani Mara.
Mitawi ametoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wa kueneza elimu ya
ozoni kwa wadau wengine ili kuongeza uelewa na juhudi za pamoja katika kuhifadhi tabaka
la ozoni, na hivyo kuokoa maisha ya binadamu, wanyama na viumbe hai mbalimbali duniani.
“Kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni ni kemikali/gesi zinazotumika katika majokofu na
viyoyozi mbalimbali, vifaa vya kuzimia moto, usafishaji chuma, utengenezaji magodoro. Ni
wajibu wetu kama Maafisa wa Serikali katika maeneo ya mipaka tusimamie vyema sheria ili
kujikinga na madhara ya kemikali hizi” amesema Mitawi.
Kwa mujibu wa Mitawi ametaja madhara ya uharibifu wa tabaka la ozone ni pamoja na
kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali yakiwemo saratani ya ngozi, mtoto wa jicho,
upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi na kuathirika kwa ukuaji wa
mimea.
Ameongeza kuwa kutokana na madhara ya kemikali hizo, Serikali imekuwa ikiendesha
mafunzo kwa wasimamizi wa sheria na maafisa wa forodha mipakani kwa kuzingatia kuwa
ndio wahusika wakuu katika kudhibiti uingizaji wa bidhaa mbalimbali mipakani zikiwemo
kemikali hizo katika maeneo yao ya kazi.
Akiwasilisha Mada kuhusu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Kanuni za Kudhibiti Kemikali
zinazoharibu Tabaka la Ozoni) za mwaka 2022, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Ofisi ya
Makamu wa Rais Bw. Dustan Shimbo amesema katika kutekeleza Itifaki ya Montreal,
Serikali imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali iliwemo Mpango wa Kuondosha Kemikali
Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni Jamii ya Hydrochlorofluorocarbons (HCFCs) ifikapo
mwaka 2030.
Ameongeza kuwa Serikali ipo katika maandalizi ya Mpango wa utekelezaji wa Marekebisho
ya Kigali ya kupunguza matumizi ya kemikali jamii ya hidrofluorokaboni ambapo mojawapo
ya shughuli zinazotelekezwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa Maafisa wa Serikali walioko
mipakani ikiwa ni utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za mwaka 2022.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mhandisi
George Ngoso amesema suala udhibiti wa kemikali na vifaa vya kemikali linahitaji nguvu ya
pamoja vaina ya wadau waliopo katika mnyororo wa thamani ili kulinda afya za binadamu na
mazingira.
Mhandisi Ngoso amesema ni wajibu wa mawakala wa forodha waliopo mipakani kujifunza
teknolojia mpya ya ukaguzi wa mizigo ikiwemo bidhaa za kemikali kuendelea na usimamizi
na udhibiti wa kemikali zinazodhibitiwa kwa kuzingatia ukomo wa matumizi wa kemikali hizo.
“Mnapaswa kuwa wazalendo na kutanguliza maslahi ya taifa na jamii inayowazunguka,
madhara ya uingizaji wa bidhaa hizi unaweza kuleta athati kuwa kwa afya za binadamu na
mazingira, hivyo tunapaswa kuhakikisha kuwa tunadhibiti kemikali hizi kutoweza kuingia
katika jamii yetu” amesema Ngoso.
Tanzania ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Vienna unaohusu hifadhi ya Tabaka la
Ozoni na Itifaki ya Montreal kuhusu udhibiti wa kemikali zinazoharibu tabaka la ozoni
ambapo Mkataba huo iliridhiwa na nchi mwaka 1993.
Katika mafunzo hayo washiriki hao walielimishwa kuhusu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira
(Kanuni za Kudhibiti Kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni) za mwaka 2022, Sayansi ya
Ozoni na athari zitokanazo na uharibifu wa tabaka la ozoni, Matumizi ya Mitambo ya
Kutambua Gesi zinazoharibu Tabaka la Ozoni.
Jumla ya Mawakala wa forodha na Wasimamizi wa Sheria 25 waliopo katika Mpaka wa
Sirari, Mkoani Mara walishiriki mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza tarehe 17 hadi 18,
2024 na kuandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.