Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Februari 17, 2024 katika
Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Boko - Dar es Salaam ameungana na
ndugu, jamaa na marafiki, katika kuuaga mwili wa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa
Kamala aliyefariki dunia tarehe 12 Febuari 2024.
Prof. Mwegoha amewasilisha salamu za pole kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu
Mzumbe na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dkt. Ali
Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Saida Yahya – Othman,
ambao kwa pamoja wamemwelezea Marehemu Balozi Kamala kama kiongozi
aliyekuwa na maono ya kimkakati katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa ndani na
nje ya nchi, kujenga amani na kuleta maendeleo kwa Tanzania kupitia nyadhifa
mbalimbali alizoshika enzi za uhai wake.
“Tukio hili si jepesi kulipokea hasa ukizingatia mahusiano mema ambayo marehemu
aliyejenga na wafanyakazi wenzake, wanafunzi na watu mbalimbali waliobahatika
kukutana naye. Pia, ni pigo kubwa kwa jamii yetu na kwa nchi ya Tanzania kwa
ujumla kupoteza kiongozi mwenye uzoefu na mchango mkubwa katika nyanja
mbalimbali hususan kwetu sisi wanataaluma” Amesisitiza Prof. Mwegoha
Amesema Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala atakumbukwa sana kwa mchango
mkubwa kwa Chuo Kikuu Mzumbe toka alipokuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi
(IDM-Mzumbe), akiwa mtu aliyeipenda sana kazi yake katika kuongoza kundi kubwa
la wanachuo na kuajiriwa kama Mkufunzi mwenye ufahamu wa hali juu katika
masuala ya Uchumi.
“Mchango wa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala bado unaishi na utaendelea
kuishi kupitia kazi nyingi za kitaaluma na kisiasa alizozifanya. Moja ya vitu
vinavyofariji ni sifa aliyokuwa nayo ya kupenda kuyaweka mawazo yake katika
maandishi. Hii inatusaidia kubaki na rejea ya mambo aliyoyafahamu, vitu
alivyoviamini na mawazo aliyoyajenga juu ya mambo mbalimbali” Amesisitiza Prof.
Mwegoha.
Awali, Paroko wa Kanisa la Mwenyeheri Isidori Bakanja Padri Emmanuel Makusalo
na Padri Florence Rutaihwa Rwehumbiza kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania
walioendesha ibada ya misa ya mazishi, kwa pamoja, wamewataka waamini na
waombolezaji kujiandaa na kifo kwa kudumu katika sala ili waweze kukikabili vema
kwa kuwa hakuna ajuaye siku wala saa.