MAKAMU WA RAIS AONGOZA VIONGOZI NA WANANCHI KUTOA HESHIMA ZA MWISHO

MUUNGANO   MEDIA
0



 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.

Philip Mpango amewaongoza viongozi na wananchi katika kutoa heshima za

mwisho kwa Waziri Mkuu Mstaafu hayati Edward Ngoyai Lowassa katika

viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam.

Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa

Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais ametoa pole kwa

familia, ndugu, marafiki pamoja na watanzania wote kwa ujumla kufuatia

msiba huo mkubwa kwa Taifa.

Makamu wa Rais amesema serikali inathamini uzalendo na mchango mkubwa

aliyoutoa Hayati Edward Lowassa katika maendeleo ya nchi kwa kuwa

alijitolea kwa dhati kulitumikia Taifa pamoja na kutumia vema karama

alizojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwatumikia Watanzania katika nyadhifa

mbalimbali alizowahi kushika. Amesema ni muhimu kila mmoja mtanzania

kujikumbusha wajibu aliyonao kwa taifa na kuyaishi kwa vitendo mambo yote

mazuri yanayotokana na maisha ya hayati Lowassa.

Amesema ni vema Watanzania kumuenzi hayati Lowassa kwa kuendelea

kuchapa kazi ili kuboresha maisha na hivyo kuchangia katika ujenzi wa Taifa

kwa kuwa alikuwa mchapa kazi hodari katika utumishi wa umma na katika

shughuli zake binafsi ikiwemo ufugaji.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa watanzania wote na hususan vijana

kumuenzi hayati Lowassa kwa kutumia fursa mbalimbali kujipatia elimu kwa

manufaa ya Taifa kwa kuwa alikua kinara katika elimu na kusimamia kwa

uhodari utekelezaji wa sera, mikakati na mipango mbalimbali ya elimu

hususan ujenzi wa shule za Sekondari kila Kata.

Makamu wa Rais amesema Hayati Edward Lowassa alikuwa mwanamazingira

hodari ambapo katika wadhifa wake wa Waziri wa Nchi - Ofisi ya Makamu wa

Rais na alipokuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

alihimiza sana uhifadhi na Utunzaji wa mazingira. Aliongoza kampeni nyingi za

upandaji miti na usafi wa mazingira. Amesema mchango wake huo

uwakumbushe watanzania wote wajibu wa msingi wa kulinda na kutunza

mazingira na hususan vyanzo vya maji ili kukabiliana na athari za mabadiliko

ya tabianchi ambazo zinaendelea kuleta madhara mengi katika Taifa na dunia

kwa ujumla.


Vilevile Makamu wa Rais amesema Hayati Edward Lowassa alikuwa na bidii

katika kumwabudu Mwenyezi Mungu akiwa msharika mzuri, akisali mara

nyingi katika kanisa la KKKT Azania Front. Amesema mfano huo ikumbushe

kuwa kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa na msingi wa mafanikio katika

familia na katika utumishi wa umma.

Makamu wa Rais amewasihi watanzania kutumia msiba huo kudumisha na

kuimarisha upendo, amani na mshikamano wa Taifa.


Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

13 Februari 2024

Dar es salaam.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)