WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KUANDAA MFUMO WA KUSIMAMIA MASUALA YA HAKI ZA BINADAMU NA BIASHARA

MUUNGANO   MEDIA
0

 

Na. Mwandishi Wetu, Arusha.

Kutokana na kukua kwa shughuli za uwekezaji zinazoweza kuleta matokeo chanya au hasi kwa haki za binadamu na watu, Wizara ya katiba na sheria inatarajia kuandaa mfumo wa kusimamia masuala ya haki za binadamu na biashara kupitia Mpango Kazi wa Haki za Binadamu na Biashara. 


Hayo yamebainishwa Jijini Arusha na Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana wakati akizindua kamati ya kitaifa ya kusimamia uandaaji wa mpango kazi wa kitaifa wa haki za binadamu na biashara.


“Ni matarajio yangu kuwa kamati hii, ninayoizundua leo, na ambayo inajumuisha makundi mbali kutoka Serikalini, Asasi za Kiraia na Sekta ya Biashara, itahakikisha kuwa Mpango Kazi huo utapambanua na kuelelezea vipaumbele na masuala yatakayoungwa mkono katika utekelezaji wa Wajibu wa Kitaifa, Kimataifa, Kikanda wa masuala ya haki za binadamu na biashara,”amesema Dkt. Chana. 


Amesema kutokana na juhudi hizo za Serikali, katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania ilifikia hadhi ya uchumi wa kipato cha kati unaohitaji juhudi za pamoja kushughulikia uwajibikaji wa biashara ambapo katika kufikia juhudi hizo imependekeza kuweka mkakati wa kutekeleza masuala ya Haki za Binadamu na Biashara ili kuchangia katika kutekeleza sera zake za Kitaifa na mipango mikakati ya nchi hasa kutekeleza mipango yake ya maendeleo pamoja na dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025.


“Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kutekeleza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu, ikiwemo katika eneo la biashara na uwekezaji na watu kwa kutekeleza Sheria, mipango, mikakati na programu zinazotafsiri upatikanaji wa haki mbalimbali za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, makundi maalumu, ikiwemo haki ya maendeleo na masuala ya mazingira,”amesema.


Sambamba na hayo Dkt. Chana ameongeza kuwa serikali inalinda, inakuza na kusimamia haki za binadamu nchini kama zilivyoatamkwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sheria, kanuni, tarataibu zilizopo na mikataba ya kikanda na Kimataifa, ambayo nchi imeridhia. 


“Kutokana na umuhimu wa eneo la haki za binadamu, Serikali kupitia Ibara ya 129 (1) ya Katiba ilianzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambayo ni tasisi huru ya kitaifa ya haki za binadamu na mchunguzi maalum (Ombudsman) yenye jukumu la kikatiba na kisheria la kuhamasisha nchini hifadhi ya  haki za binadamu na wajibu kwa jamii kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi na Mikataba ya Kimataifa na Kikandaa ambayo Tanzania imeridhia,”ameongeza Dkt. Chana.


Awali akitoa neno la utangulizi Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji mstaafu Mathew Mwaimu amesema tangu mwaka 2011 mwongozo wa kanuni za Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu na Biashara uliporidhiwa ni takribani nchi 11 za Afrika ambazo zimechukua hatua ya kuanzisha mchakato wa kuandaa mpango kazi wa kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara.


“Nchi hizo ni Kenya, Morocco, Liberia, Uganda, Ghana, Nigeria, Zambia, Msumbiji na Afrika Kusini, Siera Leone na Tanzania.  Mchakato wa kuandaa Mpango kazi katika nchi hizo umeanzishwa na kuongozwa aidha na Serikali, asasi za kiraia, Tume za Haki za Binadamu kama hii yetu na au Taasisi za Kitaaluma , katika Afrika Mashariki, nchi za Kenya na Uganda zimeshaandaa mpango huu na sasa hivi zipo katika hatua ya utekelezaji,”amesema.


Aidha ameongeza kuwa tathmini iliyofanyika Mwaka 2017 pamoja na jitihada zingine zilizotajwa kufanyika na THBUB katika eneo la biashara na uwekezaji zilibainisha kuwa ukuaji wa shughuli za uwekezaji na biashara unaenda sambamba na haki za binadamu. 


Amesema shughuli za biashara zina faida kubwa katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni, ikiwemo kukuza ajira na kipato, kukuza ujuzi na teknolojia, kuimarisha miundombinu, kufikisha huduma za kijamii kwa urahisi, kuimarisha mahusiano ya kibiashara miongoni mwa nchini duniani pamoja na kufuta umaskini.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)