Viongozi na Taasisi mbali mbali zinazohusika na kukabiliana na Maafa wametakiwa kutoa uwelewa kwa jamii juu ya majanga na jinsi ya kutumia rasilimali zilizopo katika kujikinga na maafa ili kunusuru maisha ya Raia na mali zao.
Kauli hio imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alipowahutubia Viongozi na wananchi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya kukabiliana na Maafa Duniani kilichofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Amesema kuwa lengo kuu la kuadhimisha siku ya kukabiliana na Maafa ni kuihamasisha jamii pamoja na Taasisi mbali mbali kutekeleza wajibu wao katika kupunguza uwezekano wa kukumbwa na Maafaa pamoja na kukumbushana wajibu wa kuchukua hatua za kujikinga na majanga yanayosababishwa na binaadamu, kupunguza athari kwa majanga ya kimaumbile sambamba na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali baada ya kutokea maafa.
Mhe. Hemed amefahamisha kuwa kuongezeka kwa matukio mbali mbali ya majanga yakiwemo ya matetemeko ya ardhi, upepo mkali, kuzama kwa meli na ajali za barabarani pamoja na majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika Visiwa vya Zanzibar yanasababisha kuwepo kwa jamii kubwa tegemezi na yenye uwezo mdogo katika kukabiliana na kurejesha hali wakati na baada ya maafa kutokea.
Ametoa wito kwa Taasisi zote zenye miradi ya ujenzi kuhakikisha zinashirikina na Kamisheni ya kukabiliaba na maafa na kikosi cha Zima moto na Uokozi kabla, wakati na baada ya ujenzi ili kuhakikisha uwepo wa mipango na miundombinu ya kukabiliana na majanga .Sambamba na hayo amewataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima pamoja na Jeshi la Polisi liendelee kusimamia sheria za usalama barabarani ikiwemo kuwachukulia hatua wale wote wanaokiuka sheria hizo pamoja na kukata bima kwa wafanyabiashara, wamiliki wa vyombo vya usafiri na mitambo ili kuweza kurejesha hali pindi maafa yatakapotokea.
Aidha amezitaka Serikali ya Mikoa na Wilaya kusimamia ujenzi kwa mipango ili kuepusha ujenzi holela katika jamii hatua ambayo itasaidia kuweza kupambana na majanga yatakapotokea.