SHIMIWI YATOA FURSA KWA WATUMISHI KUTEMBELEA HIFADHI YA RUAHA.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na. Asila Twaha, Iringa.

Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za SERIKALI (SHIMIWI) limetoa nafasi kwa watumishi wote walioshiriki michezo inayoendelea Mkoani Iringa kutembelea hifadhi ya Taifa RUAHA ili kujifunza na kuwa mabalozi wa  kutangaza vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo mara watakaporejea kwenye maeneo yao ya kazi.


Watumishi  zaidi ya 600 wakiwemo wa TAMISEMI  Oktoba 7, 2023 kutoka katika Wizara, Taasisi na Idara za Serikali wametembelea hifadhi ya RUAHA na kujifunza vivutio vingi vilivyopo ikiwemo kuona na kujifunza tabia za wanyama wakubwa 5 ambao husifika kwa uzuri lakini pia ukali wao na jinsi wanavyoweza kutawala maeneo yao.


Wanyama hao maarufu kama (Big Five)  ni Simba, Tembo, Nyati, Chui na Faru wanapatikana katika hifadhi hiyo ambao wamekua kivutio cha watu wengi kwenda kutembelea hifadhi hiyo.


Mbali na kuwa na  vivutio vizuri tofauti na hifadhi nyengine kwa kuwepo na wanyama aina simba wengi, wanyama aina ya tandala ambao hao ni kivutio kwa watu wengi lakini pia ni hifadhi yenye utulivu ambapo wanyama wanapata muda wa kufanya shughuli zao za kiwindaji bila ya kuwa na muingiliano na makazi ya watu. 

Kwa upande wa Katibu wa TAMISEMI Sports Club Alex Morice amesema, nafasi waliyoipata kutembelea hifadhi hiyo imekua ya kipekee  kwa wanamichezo  wote. 


Amesema tunaushukuru uongozi wa  SHIMIWI kwa kuweka ratiba hiyo sababu ushiriki wetu katika michezo siyo tu kufahamiana, kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kikazi na kimichezo bali imetuongezea uelewa  tabia za wanyama na kuona vitu vizuri ambavyo Mungu ameipatia nchi yetu.


"Kama kauli mbiu ya uhifadhi inavyosema Tumerithishwa na sisi hatuna budi ya  kuwarithisha watoto  na vizazi vyetu" amesema Morice.


Hifadhi ya RUAHA ina ukubwa wa kilomita za mraba 20,226.






Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)