NAIBU WAZIRI MWINJUMA AIELEKEZA COSOTA KUPATA MPANGO KAZI WA KUKUSANYA MIRABAHA.

MUUNGANO   MEDIA
0

NAIBU Waziri Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma atoa maelekezo kwa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kuhakikisha inapata mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu kutoka kwa Kampuni ya Kukusanya Mirabaha ya kazi za Muziki iliyopewa Leseni ijulikanayo kama Tanzania Music Rights Society (TAMRISO) na kuhakikisha Kampuni hiyo imewasilisha mfumo wa ufuatiliaji wa matumizi ya kazi za Muziki katika maeneo mbalimbali kabla ya mwishoni mwa mwezi Oktoba 2023.


Mheshimiwa Naibu Waziri huyo ametoa agizo hilo leo Oktoba 17, 2023 katika kikao chake na Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Bi.Doreen Anthony Sinare alipotembelea Ofisini kupata mrejesho wa utendaji wa TAMRISO.


" Suala la TAMRISO kuwa na mfumo ni jambo la muhimu sana sababu mfumo ndiyo unasidia kujua nani amepata kiasi gani kulingana na matumizi ya kazi yake na Wasanii wengi wemekuwa wanalalamika hili hivyo ni lazima walete taarifa ya mfumo huo," alisema Naibu Waziri Mhe. Mwinjuma.


Pamoja na hayo Mhe. Naibu Waziri Mwinjuma ameipongeza COSOTA kwa kukamilisha mchakato wa kuwezesha makusanyo ya Tozo ya Hakimiliki ( Blanktape Levy) kuanza kufanyika, pia ameeleza kuwa Wizara itaendele na mchakato wa kuomba bunge kuridhia baadhi ya vifaa ambavyo havijaingizwa kwenye orodha ya awali vyenye matumizi makubwa katika kazi za sanaa ikiwemo Kompyuta, Simu, Flash, Harddrive, Vishikwambi na vinginevyo. Lengo likiwa ni Wasanii waweze kunufaika na tozo hii na itakayowasaidia kiuchumi.


Naye Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Doreen Anthony Sinare alieleza kuwa yeye na Mwenyekiti wa Bodi ya Ofisi ya Hakimiliki Ndg. Victor Tesha wamepanga kufanya kikao na viongozi wa TAMRISO na wiki hii kupata taarifa ya mpango kazi wao na utekelezaji, hivyo mara baada ya kikao hicho atawasilisha taarifa Wizarani.


"Tumetoa tangazo la kuongeza siku za wadau kuomba Leseni ya Kampuni ya Kukusanya Mirabaha kwa madaraja ambayo yalikuwa bado hayajaomba kama wadau wa Filamu, Sanaa za Ufundi, Wachapishaji wa Vitabu na Sanaa za Maonesho na mwisho wa kuwasilisha maombi hayo ni tarehe 02 Novemba, 2023." alisema Doreen.





Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)