Mary Clemence, Katavi.
Bodi ya pamba Tanzania imeanza mchakato wa kuirasimisha Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kuwa kitalu cha uzalishaji mbegu bora za pamba ili kuwasaidia wakulima kuzipata kwa urahisi na kwa bei nafuu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Pamba Tanzania James Shimbe amebainisha hayo kwenye kikao cha wadau wa pamba cha kujadili maendeleo ya zao hilo kilichofanyika wilayani humo.
Shimbe amesema wamefikia hatua hiyo kutokana na Halmashauri hiyo kupiga hatua kubwa katika uzalishaji wa mbegu bora za pamba nchini.
“Zinafuata utaratibu unaosimamiwa na ASA, TOSIC na TARI wasimamizi tasnia ya pamba nchini, elimu inaendelea kutolewa wakulima wazalishe kwa tija, awamu hii mmezalisha zaidi ya asilimia 25”amesema Shimbe akaongeza.
“Mwaka jana mmezalisha kilo milioni nne na laki mbili kwa musimu wa 2020/2022 na 2023 hadi kufikia sasa mmezalisha kilo milioni tano laki tatu na themanini ni uzalishaji mzuri,”
Msimamizi wa shamba la Kilimi Nzenga mkoani Tabora la Wakala wa mbegu bora za kilimo (ASA) Jacob Chiwanga amesema wanayo mashamba 18 nchini yanayotumika kuzalisha na kusambaza.
“Tanganyika tuna shamba Luhafwe jipya ni sehemu mhimu tunayotarajia kulima mbegu, mchakato unaendelea wa kufungua shamba na kuzalisha tuongeze wigo wa usambazaji ukanda huu,”amesema Chiwanga.
Mratibu wa utafiti zao la pamba kitaifa kutoka TARI Ukiriguru jijini Mwanza Dakta Paul Saidia amesema tija ya uzalishaji wa pamba nchini ni ndogo.
“Mkulima anavuna kilo mia tatu hadi mia nne kwa ekari moja, Katavi tija ipo juu kidogo kutokana na maeneo yalivyo wanapata kilo 800 hadi 900,”
“Mbegu iliyogunduliwa na TARI, UKM68 tija yake inaanzia kilo 1200 kwa ekari moja, tumebaini ugonjwa wa vuvuzali unaoathiri zaidi mimea, tatizo hili Katavi ni dogo sana,”amesema Saidia.
Mkulima wa pamba wa kijiji cha Majalila Abdallah Kakoso amesema utaratibu wa kuwa na kitalu cha kuzalisha mbegu utakuwa na manufaa kwa wakulima.
“Mbegu zitapatikana kwa wingi na kwa urahisi zaidi,lakini pia bei itapungua, awamu hii kilo moja nasikia inauzwa sh 1400 mfuko mmoja sh 28,000 na zinatoka mbali,”“Wapo wakulima
"wanaohitaji kulima lakini wanashindwa kumudu gharama,tunaishukru serikali kwa hatua hiyo tutaongeza uzalishaji,”amesema Kakoso.
Naye Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amewasisitiza watalaam kuhakikisha wanawasimamia wakulima waongeze uzalishaji na ubora unaokidhi vigezo.
“Mhe.rais Samia Suluhu ameweka nguvu kubwa ili tupate fedha za kigeni tuongeze dola katika nchi yetu pamba inapouzwa nje, hivyo tuzalishe kwa tija,”amesema Buswelu.
Kutokana na ongezeko la wakulima wa zao la pamba wilayani Tanganyika kiwango cha usambazaji mbegu kimeongezeka kutoka kilo 500 za awali hadi kufikia zaidi ya kilo 500.