SERIKALI YADHAMIRIA KILIMO CHA KUJIKIMU KUWA KILIMO CHA BIASHARA

MUUNGANO   MEDIA
0

Serikali imepanga kubadilisha dhana ya kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara na mabadiliko haya yanafanyika kwa kuzingatia malengo ya kitaifa kama yalivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025


Kauli hiyo imetolewa Agosti 4, 2023 na Waziri wa Utamaduni ,Sanaa na Mchezo Mhe. Dkt Pindi Chana wakati akifungua Kongamano la Mtama kwa wakulima na wadau mbalimbali wa zao hilo kwenye maonyesho ya Nanenane katika viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma. 


Mhe. Chana amewataka wakulima wa zao la Mtama wa Mikoa ya Kanda ya kati kuweka mikakati mathubuti ya zao hilo ili kuleta mageuzi kwa ajili ya biashara na kuachana na dhana ya chakula cha njaa kutokana na hali ya hewa ya Mikoa hiyo. 


Ameendelea kwa kutoa wito kwa wakulima kuzalisha chakula chakutosha na kuachana na kilimo cha mazoea ili kuachana na dhana ya kuagiza chakula nje ya nchi kama ilivyo dhamira ya serikali inaendelea kufanya mageuzi kwa wananchi wake. 


"Mikoa ya Kanda ya Kati kama ilivyo kwa nchi na dunia nzima inakabiliwa na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo hayajatoa mwelekeo wowote wa kama hali ya hewa itabadilika katika misimu mingine itakayofuata” ameeleza Mhe. Chana.

Katika hatua nyingine Mhe. Chana amewataka washiriki wa Kongamano la Mtama kuwa mabalozi kwa wakulima wengine kwa kuwapatia elimu na mafunzo watakayo yapata ili kuwasadia kulima kilimo cha kisasa, bora na chenye manufaa katika maisha ya sasa na baadae.



Ameendelea kutoa rai kwa watanzania kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya teknolojia mbalimbali za kilimo zinazoendelea kutolewa na wataalamu katika kipindi hiki cha maonyesho ya nane nane. 


Kwa Upande Wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Peter Selukamba amewasihi wakulima kujifunza mbinu bora ambazo zitawasaidia kulima zao hilo kwa wingi pamoja na kuondoka na maazimio ambayo yatakuwa na tija katika kufanyikisha kilimo bora.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)