Na. Asila Twaha, Pwani.
Mratibu wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ndugu Joel Mhoja amesema, jumla ya washiriki 4,104 watanufaika na mafunzo hayo kupitia mradi wa Kuboresha Mazingira ya Ujifunzaji katika Elimu ya Awali na Msingi (BOOST).
Mhoja ameyasema hayo Juni 30, 2023 wakati mafunzo yakiendelea yenye lengo la kuwajengea uwezo walimu kuhusu Matumizi ya Njia na Vifaa vya Mtaala wa Elimu ya Awali vilivyoboreshwa kwa Walimu wa Elimu ya Awali, Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata.
Amesema washiriki hao 4,104 watakaopatiwa mafunzo wakimaliza mafunzo yao watakua ni balozi wazuri kwa wenzao na watatakiwa kuwajengea uwezo wenzao mara watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi.
"Mafunzo haya yatakuwa na mada ya ubunifu, utengenezaji na ufaraguzi wa zana kutokana na makunzi yanayopatikana kwenye mazingira ya shule na sio mafunzo ya nadharia pekee.
Mhoja amesema Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini kuhusu Matumizi ya Njia na Vifaa vya Mtaala wa Elimu ya Awali vilivyoboreshwa ni sehemu ya utekelezaji wa afua mojawapo katika Mradi BOOST.
Amesema, pamoja na Serikali kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya shule lakini pia imeweka kipaumbele katika kuboresha umahiri wa walimu kwa kuwajengea uwezo na kuwaongezea ujuzi katika kumudu njia na mbinu bora za kujifunzia na kufundishia.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanaendelea katika vituo 22 yakihusisha walimu kutoka mikoa yote 26 na amesisitiza kuwa Serikali inaamini kuwa walimu waliopatiwa mafunzo hayo wataenda kuleta mabadiliko chanya katika elimu ya awali na elimu ya msingu kwa ujumla.
"Hii ni kwa sababu ukitaka kuboresha elimu ni lazima kuanza na E
elimu ya awali.
Naye Mwalimu wa Shule ya Awali Temeke- Dar es Salaam Mwalimu Mwajuma Mlezi amesema, mafunzo wanayopatiwa yatawajengea umahiri utakaowezesha kuleta mabadiliko katika matumizi ya mbinu bora katika ufundishaji na yatawaongezea ujuzi wa kufaragua zana za kufundishia zilizopo katika maeneo ya kazi.