Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila) imesema itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi ya Vision Care kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma za matibabu ya macho hospitalini hapa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji Prof. Mohamed Janabi wakati akipokea msaada wa mashine ya kusaidia kurekebisha saizi ya kioo anachotakiwa kuwekewa mgonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji wa kutoa mtoto wa jicho chenye thamani ya takribani TZS. 23 Mil.
Prof. Janabi ameongeza kuwa MNH inathamini mchango wa taasisi hiyo katika kuboresha huduma ambapo imekuwa ikiisadia katika eneo la vifaa tiba na kuwajengea uwezo wataalamu wa macho tangu mwaka 2020.
“Pamoja na kuwekeza katika kununua vifaa tiba, hospitali pia imeendelea kuthamini katika kuwajengea uwezo wataalamu ili waweze kuongeza ujuzi na weledi katika maeneo ya ubobezi kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia” amesema Prof. Janabi.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Macho, Dkt. Joachim Kilemile amesema kifaa hicho kitasaidia kuboresha huduma kwakuwa atawekewa kioo kulingana na saizi yake badala ya kukadiria na pia kutapunguza uhitaji wa mtu kuvaa miwani baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mtoto wa jicho.
Aidha Dkt. Kilemile amesema MNH kwa kushirikiana na Madktari Bingwa kutoka Korea Kusini na Marekani itafanya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa njia ya matundu madogo (phacoemulfication surgery).
Naye, Rais wa Vision Care nchini Marekani ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho, Prof. Lisa Park ameupongeza uongozi wa MNH kwa matumizi mazuri ya vifaa wanavyowapatia na kuwajangea uwezo wataalam wake.
Prof. Park ameongeza kuwa Muhimbili ni hospitali kubwa ambayo wataalam wake wanatumika kuwajengea uwezo wataalam wa hospitali zingine nchini ndio maana Vision Care imeendelea kushirikiana na Muhimbili katika kuwajengea uwezo wataalam na kuwapa vifaa tiba.