Wananchi wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wametakiwa kuuchukulia mradi wa Uboreshaji usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) kama fursa na kutoa ushirikiano thabiti ili kufanikisha utekelezaji wake na kutatua changamoto mbalimbali za ardhi zinazoikabili Wilaya hiyo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge akifungua Mkutano wa wadau kujadili mpango wa matumizi ya Ardhi uliofanyika leo tarehe 11/07/2023 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Mhe. Kaminyoge amesema kuwa Wilaya ya Maswa imepata bahati ya kuteuliwa kuwa miongoni mwa Wilaya chache zilizopata nafasi ya kutekeleza mradi huo hivyo amewaomba watekeleze mradi huo kwa ufanisi mkubwa pamoja na kutoa ushirikiano wa karibu kwa wataalam ili kufanikisha dhima ya mradi huo.
“Maeneo mengi yalitamani kupata fursa kama hii lakini kutokana na uchache wa rasiliamli hawakufanikiwa kufikiwa na mradi hivyo nawashauri tuitumie fursa hii kikamilifu kwa maendeleo ya Wilaya yetu ya Maswa na Mkoa wetu wa Simiyu kwa ujumla” alisema Mhe. Kaminyoge.
Aidha Mhe. Kaminyoge ameongeza kuwa utekelezaji wa mpango wa matumizi ya Ardhi kwa Wilaya ya Maswa utaleta matokeo chanya katika kuchochea maendeleo ikiwa ni pamoja na kuleta usalama wa milki za ardhi, kukuza huduma za kiuchumi na kijamii, kuboresha hifadhi ya mazingira na kumaliza migogoro itokanayo na ardhi.
Hata hivyo amewataka watendaji wa Kata kuwa karibu na wataalam ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo na hasa uandaaji wa mipango ya matumizi ya Ardhi ya vijiji ambao umekwishaanza katika vijiji 8 vya Wilaya hiyo.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi umefanikiwa kuandaa mipango ya matumizi ya Ardhi ya Wilaya katila Wilaya 5 ambazo ni Chamwino, Mbinga, Songwe, Maswa, Mufindi na Longido. Aidha hatua inayofuata ni kuandaa mipango ya matumzi ya Ardhi ngazi za vijiji katika Wilaya hizo.