MAAFISA LISHE TOENI ELIMU YA LISHE KWA JAMII.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Dkt. Charles Mahera amewataka maafisa lishe nchini kutoa elimu kwa jamii ili kuepuka udumavu kwa watoto. 


Dkt. Mahera ametoa wito huo leo Mkoani Iringa katika ziara ya kikazi inayofanywa kwa pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dtk.Grace Magembe kukagua utoaji na ubora wa huduma kuanzia ngazi ya msingi hadi rufaa, ambapo wamekagua hali ya utoaji Huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Iringa na Hospitali ya Halmashauri ya Iringa Frelimo.


Dkt. Mahera amesisitiza maafisa hao kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya udumavu kwa watoto hasa wenye umri chini ya miaka nane na namna ya kuwatangenezea chakula chenye lishe. 



“Tujitahidi kutoa elimu kwenye jamii zetu kwani madhara ya udumavu katika umri mdogo unapelekea watoto kutoelewa vizuri darasani pindi wanaposoma na kuleta madhara ya kudumu pale wanapofikisha umri mkubwa”, ameeleza Dkt. Mahera. 


Hata hivyo Dkt. Mahera amewataka maafisa hao kuweka mikakati madhubuti ya kusaidia jamii katika kuondokana na janga la udumavu kwa watoto wasiopata lishe bora ambalo lina madhara makubwa katika ukuaji wa mtoto. 


“Tafuteni mbinu ya kutoa elimu kwa jamii na ilete tija juu ya kumaliza udumavu tuwe na asilimia sifuri na haya yote yataletwa na mikakati madhubuti ya mtakayo kuwa mmeweka”, ameeleza Dkt. Mahera.  

Sambamba na hilo Dkt. Mahera amewataka watumishi wote kuheshimiana na kushirikiana ili sekta ya Afya itoe huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia miongozo ya utoaji wa Huduma za afya. 


Pia Mahera ameongeza kuwa wafamasia wasimamie dawa kwa uangalifu ili wananchi wapate huduma na zenye uhakika kulingana na uwekezaji uliofanywa na serikali yao.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amezitaka Hospiatali za Rufaa nchini kuhakikisha zinatoa huduma za utengamao na tiba mazoezi ili kuwezesha wananchi wenye uhitaji wakiwemo watoto wenye ulemavu kuishi maisha yenye ubora na kuweza kujihudumia wao wenyewe


"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kununua vifaa tiba vya kisasa kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa, ni lazima tuwe na mpango wa matengenezo, ili vikiharibika kidogo visiwekwe stoo kwani itakuwa ni hasara kwa serikali na kuwanyima wananchi huduma”, ameeleza Dkt. Grace.


Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)