DMO’s NA MA DED WATAKIWA KUSHIRIKIANA KULETA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA

MUUNGANO   MEDIA
0

Na Mwandishi Wetu, OR-TAMISEMI.

Waganga Wakuu wa Halmashauri nchini wametakiwa kushirikiana kwa karibu na Wakurugenzi wao ili kuleta ufanisi katika kuwahudumia wananchi.


Agizo hilo limetolewa leo Jijini Mbeya na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Charles Mahera wakati akizungumza na watumishi wa sekta ya afya wa mkoa huo.


Dkt. Mahera amesema kuwa watendaji hao wakishirikiana katika kutekeleza majukumu yao wataleta ufanisi katika kutoa Huduma bora kwa mwananchi.

“Natoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani mpaka sasa ametoa kiasi cha shilingi Bilioni 900 kwa ajili ya sekta ya afya”, ameeleza Dkt. Mahera


Amesema kuwa uwekezaji wa wataalamu, ujenzi wa miundombinu, vifaa na vifaa tiba, nyumba za watumishi, dawa na vitendanishi lengo ni wananchi kupata Huduma bora hivyo ni wajibu watendaji hao kushirikiana ili kuweza kufikia malengo.


Aidha amewataka makatibu wa afya katika vituo vya kutolea Huduma za afya kufanya majukumu yao kwa ufasaha ili kuleta matokeo katika nafasi zao.


“RCHMT na CHMT fanyeni tekelezeni majukumu yenu ili kuleta ubora wa Huduma katika vituo vya kutolea Huduma na lazima mlete matokeo chanya yatakayo mgusa mwananchi moja kwa moja”, ameelekeza Dkt. Mahera 


Vile vile amewataka kuhakikisha wanashirikisha jamii katika vijiji na kata ili kujua nini kinafanyika katika maeneo yao na kuwapa nafsa wananchi kushiriki katika maendeleo mbalimbali katika maeneo yao.

Ameongeza kuwa kila Halmashauri nchini itapata magari mawili ya kubebea wagonjwa 


Lakini pia ameeleza kuwa serikali inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi ambapo mpka sasa nyumba za watumishi wa afya 150 zimejengwa hivyo boresheni Huduma za afya katika utendaji wenu.


“DMO hakikisheni mnasimamia miongozo, sera, na kanuni katika kuongoza vituo na dawa zipatikane kwa wakati”, ameelekeza

Hivyo amewataka kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa dawa, Huduma na vifaa tiba vilivyopo katika vituo vyao na kuhakikisha Huduma bora zinapatikana katika vituo.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)