Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida imeweza kutamatisha Bonanza la michezo lililokuwa na lengo la kuelimisha na kutoa huduma za afya kwa vijana katika manispaa ya Singida
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe. Thomas Apson akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida ambaye ni mgeni rasmi ameipongeza Wizara ya Afya kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na ofisi ya mkuu wa mkoa kwa kuweza kuwakutanisha vijana kupitia Bonanza na kupatiwa elimu ya afya na huduma mbalimbali za upimaji afya ambapo zaidi ya vijana 1553 wamefikiwa.
"Vijana ni nguvu kazi ya taifa katika nchi yetu vijana wanategemewa katika maendeleo ya nchi yetu, ili Tanzania iwe taifa lenye nguvu ni wazi inahitajika jitihada kubwa katika kuwekeza katika afya za vijana na elimu, jambo hili litawezesha kuwa na vijana wenye nguvu ya kuwajibika katika maisha yao wenyewe, familia zao na taifa kwa ujumla," amesema Apson
Aidha Mhe. Apson amewataka vijana kuacha matumizi ya tumbaku, pombe, dawa za kulevya na shisha kwani hupelekea vijana wengi kuwa na tatizo la afya ya akili na kupoteza nguvu kazi ya taifa pamoja na kuendelea kujikinga na maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono na kufanya mazoezi kwa wingi na kula vyakula bora kwa afya ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
Naye Bi Jesca Masanja afisa kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana amewataka vijana kutumia vyema elimu ya afya waliyopewa na wataalamu wa afya ili kuweza kutunza afya na kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kuweza kuepukana na magonjwa mbalimbali.
Katika kutamatisha Bonanza hilo washindi waliofanya vizuri wamepatiwa zawadi mbalimbali kama pongezi na kuwahamasisha kuendelea kufanya vizuri zaidi katika michezo ili kuboresha afya za mwili.
Aidha Mabonanza ya uelimishaji na upimaji wa afya kwa vijana yanaendelea katika halmashauri za wilaya ya Iramba na Singida hadi tarehe 17 mwezi huu.