Na Emanuel Kawau.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika
Kongamano la kitaifa la kujenga uelewa kuhusu athari zitokanazo na sauti zilizozidi viwango katika nyumba za ibada.
Akizungumzia na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam Mwenyekiti Wa jumuiya ya Maridhiano na amani Nchini Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum amesema Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) na Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC) na linatarajiwa kufanyika Juni 12 mwaka huu (2023) Jijini Dar es salaam katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).
Aidha amewaomba na kuwaalika viongozi wote wa Dini na madhehebu yote,kuhudhuria katika Kongamano hilo ambalo mada Tisa zitawasilishwa ikiwemo "utiifu wa mamlaka kwa mujibu wa Biblia,Qur'an na Sunna,uchungaji wa haki za wengine kwa mujibu wa Biblia, Qur'an na Sunna,sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake,athari zitokanazo na sauti zilizozidi viwango,usimamizi wa mipango miji pamoja na uelewa kuhusu sheria na kanuni za usajili wa asasi za kiraia"
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Eng. Samuel Gwamaka Mafwenga amesema Kongamano hilo linawalenga viongozi wote wa Dini na mila hivyo wanawaomba viongozi wote hao kufika katika Kongamano hilo na kupata uelewa wa pamoja.
Aidha amesema Kongamano hilo ni sehemu moja wapo ya majukumu ya NEMC katika kutoa Elimu na uelewa kwa Umma.