KAMPEINI YA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA INALENGA KULINDA NA KUKUZA UPATIKANAJI WA HAKI - MHE HEMED.

MUUNGANO   MEDIA
0


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kampeni ya huduma ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia inalenga kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kupitia huduma za msaada wa kisheria Nchini.

Ameyasema hayo wakati akizindua kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Mkoa wa Mjini Magharibi katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar. 

Ameeleza kuwa kampeni hiyo itaimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wasiojiweza ,wanawake, watoto pamoja na makundi mengine yanayoishi katika mazingira magumu ,kuimarisha amani na utulivu na kuleta utengamano wa Kitaifa.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewaagiza wanaohusika na utekelezaji wa Kampeni hiyo kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi za kupiga vita na kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia, udhalilishaji na migogoro ya ardhi vitendo ambavyo vimekua vikijitokeza katika jamii.

Aidha amewapongeza wadau mbali mbali wakiwemo Wasaidizi wa Sheria, Jeshi la Polisi, Mahkama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka kwa kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake kwa mujibu wa Sheria juhudi ambazo zinaleta taswira njema kwa Wananchi kuwa na imani na wadau hao.

Nae waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Harun Ali Suleiman amesema Kampeni hiyo itasaidia kupunguza dhulma, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia katika jamii.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Idriss Kitwana Mustafa amesema Serikali ya Mkoa itakuwa karibu na wananchi katika kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa ipasavyo kwa lengo la kumuunga Mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia imezinduliwa leo kwa lengo la kuwafikia wananchi hasa wasio na uwezo ikiwa na kauli mbiu isemeyo "Msaada wa kisheria kwa haki, usawa, amani na maendeleo "
Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)