Wazazi/walezi wametakiwa kuona umuhimu wa chanjo.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na Emmanuel Kawau.

Wazazi na walezi nchini wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanapatiwa chanjo zote ili kuimarisha kinga za miili yao kwani chanjo huokoa zaidi ya Vifo milioni mbili mpaka milioni tatu vya watu  hususani watoto kila mwaka.


Wito huo umetolewa leo na Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Ilala Omary Kumbilamoto katika semina kwa wanahabari jijini Dar es salaam kuhusu huduma za Chanjo nchini ambapo amesema chanjo inauwezo wa kuzuia magonjwa mbalimbali kwa mtoto hivyo kumkinga dhidi ya ugonjwa,ulemavu na hata kifo.



"Mtoto asipopatiwa chanjo anaweza akakumbwa na magonjwa ya mlipuko kama Polio,surua na rubella na kuweza kumsababishia ulemavu au hata kifo" Amesema Kumbilamoto.


Aidha Kumbilamoto amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wakike walio chini ya miaka 14 wanapatiwa chanjo ya Saratani ya shingo ya mlango wa kizazi.



Kwa upande wake Afisa Mpango wa Chanjo Taifa kutoka Wizara ya Afya  Lotalis Gadau amesema kuanzia mwaka 2000 mpaka 2019 kiwango cha huduma za chanjo kiliongezeka kwa kiasi kikubwa kwa takribani asilimia 95% na mwaka 2020 mpaka mwaka 2021 kiwango kilishuka na kufikia asilimia 81% kutokana na Mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona UVIKO-19.



"Baada ya mlipuko wa Uviko-19 Watu wengi waliogopa kufika kwenye vituo vya Afya ili kupata Chanjo wakihofia watoto wao na wao wenyewe kupata UVIKO-19" Amesema Gadau.


Amebainisha kuwa kutokana na Mdororo huo wa mwitikio wanajamii kuwachanja watoto wao mwaka 2022 kuliibuka mlipuko wa ugonjwa wa surua na Watoto Takribani 3,923 walibainika kupata ugonjwa huo.


Gadau amebainisha kuwa Mpango wa Taifa wa Chanjo umekuwa ukihakikisha wanajiunga na Kampeni nyingine za Afya ikiwemo,kampeni ya HIV,Malaria na RCH  ili kutoa Elimu ya chanjo na chanjo.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)