WAANDISHI WATAKIWA KUWA MABALOZI WA DART.

MUUNGANO   MEDIA
0

 

Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI

NAIBU katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Dkt.Charles Msonde amewataka waandishi wa habari nchini kuendelea kuuhabarisha umma juu ya miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha na kurahisisha maisha ya watanzania kama ilivyo kwa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka(DART). 


Dkt.Msonde ameyasema hayo Mei 18, 2023 jijini Dodoma alipokuwa akifunga mafunzo elekezi kwa waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa mradi wa DART kwa niaba Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi.

Naibu Katibu huyo amesema Wakala huo ni muhimu kwa usafiri wa Jiji la Dar-es-salaam hivyo ni jukumu la waandishi wa habari kuhakikisha  mpango mkakati wa DART unaeleweka kwa wadau ili kupunguza changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika uendeshaji wa Wakala huo. 


Amewataka waandishi hao kuhakikisha wanaeleza mafanikio yaliyofikiwa na wakala huo kwa wadau  ili kuleta mafanikio makubwa katika nchi ya Tanzania na hasa wananchi wanapokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu miradi mbalimbali ya serikali.

“Lengo kuu la mafunzo ni kuwajengea uelewa wa pamoja  kuhusu namna mradi wa  unavyofanya kazi, miundombinu yake ,changamoto zilizopo na namna bora ya utatuzi wa changamoto hizo  hivyo ni wajibu wenu kuuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa  kazi za wakala huu,”amesema. 


Amewaasa kuwa mabalozi wazuri wa mradi na pale inapotokea mtu anatoa taarifa zisizo sahihi za mradi kuhakikisha wanakuwa  mstari wa mbele katika kusaidia kutoa ufafanuzi, 

“Niwaombe mkawe mabalozi wazuri wa miradi mingine inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi mahiri wa Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”amesisitiza Dkt. Msonde.


Aidha, ametoa  rai kwa Taasisi nyingine hasa zile ambazo ziko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuona umuhimu wa kuwashirikisha waandishi wa habari katika shughuli zao ili kufikisha taarifa kwa wananchi.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)