Na. Gideon
Gregory, Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Jaji mstaafu Mathew Mwaimu amesema kuwa Tume hiyo inaanza kufanya uchunguzi
juu ya kifo cha Bi. Nusura Hassan Abdallah, aliyekuwa mwanafunzi wa chou kikuu
cha Dodoma (UDOM), shahada ya kwanza ya sanaa katika Elimu (BA.Ed) katika Ndaki
ya Insia ya sayansi ya chou hicho kilichotokea wiki mbili zilizo pita.
Jaji mstaafu
Mwaimu ameyasema hayo leo Mei 10,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na
vyombo vya Habari na kubainisha kua uchunguzi huo utaanza mara moja ambapo
kwasasa mchakato bado unaendelea na mara watakapo maliza uchunguzi huo watatoa
taarifa juu ya kile kilichotokea.
Amesema lengo la
kufanya uchunguzi huo ni kupata ukweli kuhusiana na tukio hilo na kuondoa
mkanganyiko uliopo na maneno kuwa mengi.
“Tume imeona
taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari hususani mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma Bi Nusura Hassan Abdallah aliyekuwa
mwananfunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo hicho. Kwa mujibu wa taarifa,
imedaiwa kuwa Bi Nusura Hassan Abdallah alifariki katika hospitali ya Faraja,
huko Himo mkoani Kilimanjaro,
kwa
hali yoyote ile taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo ni za kusikitisha kwa kuwa
kifo hicho, iwe kwa sababu yoyote ile, kimekatisha ndoto ya maisha yake na haki
yake ya kupata elimu ya juu,”amesema.
Amesema Tume
hiyo
inatambua kuhusu kuwepo kwa vyombo vinavyoshughulikia masuala ya haki jinai
hususani
Jeshi la Polisi na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambapo katika mazingira ya
kawaida vyombo hivyo vinahusika kulishughulikia suala hilo na wanatambua hilo na tume
inavipa heshma vyombo hivyo katika utekelezaji wa majukumu yake na kazi kubwa
ambayo vinafanya.
“Hata
hivyo, kunapotokea mashaka kutoka kwa wananchi kuhusu jambo lolote
linaloashiria uvunjwaji wa haki za binadamu au mashaka ya haki kutokutendeka,
Tume inayo mamlaka ya kufanya uchunguzi juu ya jambo hilo kwa mujibu wa Katiba
na Sheria ya Tume kwa kuwa inalo jukumu la kutetea na kulinda haki za binadamu
nchini,”amesema.
Aidha, ameongeza
kuwa
kwa mujibu
wa Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Sura ya 391 Tumehiyo ina
mamlaka ya kuanzisha uchunguzi wake yenyewe juu ya malalamiko yanayoashiria
uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora pasipo
kusubiri kuletewa malalamiko.
“Kwa
muktadha huo Tume imeazimia kufanya uchunguzi wake huru kwa madhumuni ya
kubaini ukweli kuhusu matukio hilo,”ameongeza.
Amesema Tume hiyo
inachunguza mambo mengi sio tu, tukio hilo bali imekuwa ikichunguza matukio na
matukio mengine yanayokiuka misingi ya haki za binadamu.
Ikumbukwe kuwa kifo
cha Nusura Hassan Abdallah kilidhibitishwa na kitengo cha masoko na mawasiliano
cha Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Mei 5,2023 baada ya kupokea taarifa kutoka kwa
mwanafunzi ambaye alikuwa anasoma naye kuwa amepokea taarifa kutoka kwa mtu
aliyejitambulisha kuwa mjomba wake marehemu ikimjulisha kuwa Nusura amefariki
dunia akiwa anapatiwa matibabu katika hospitari ya Faraja iliyopo Himo,
Kilimanjaro.