Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi mfumo wa kuwasajili Diaspora wenye asili ya Tanzania Kidigitali (Diaspora Digital Hub).
Akizindua rasmi mfumo huo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Mashariki, Mhe. Dkt Stergomena Tax (Mb.) alisema mfumo huo utasaidia Serikali kupata taarifa sahihi za Diaspora wake katika masuala mbalimbali yanayohusu Diaspora ambao ushiriki wao kwenye kujenga uchumi wa Taifa umeendelea kukua siku hadi siku.
“Mfumo huu utaisaidia Serikali kupata taarifa sahihi za Diaspora wake, utawezesha Diaspora kufahamu na kupata taarifa zinazohusu masuala mbalimbali ya Diaspora ambapo tunashuhudia ushiriki wa Diaspora katika kujenga uchumi wa Taifa letu ukiendelea kukua siku hadi siku,” alisema Dkt. Tax.
Amesema mchango wa Diaspora katika uchumi unaonekana kupitia takwimu zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania ambapo katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 Diaspora walituma nchini Dola za Marekani Milioni 569.3 na mwezi Januari hadi Desemba 2022 walituma nchini kupitia vyanzo rasmi Dola za Marekani Bilioni 1.1 ambazo ni sawa na Shilingi Trilioni 2.6.
Aliongeza kuwa Diaspora hao kwa mwaka 2021 walinunua nyumba na viwanja nchini zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.3 na mwaka 2022 walitumia Shilingi Bilioni 4.4 kununua Nyumba na Viwanja nchini.
Alisema Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT-AMIS), unaonesha kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2022 Diaspora waliwekeza Shilingi Bilioni 2.5 katika mifuko mbalimbali ya UTT- AMIS.
Awali akizunguma katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge – Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa (Mb), alisema kuuanzishwa kwa mfumo wa kuwatambua Diaspora wenye asili ya Tanzania ni jambo muhimu litakaloiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi za Diaspora wake.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo alitoa wito kwa Diaspora wautumie Mfumo huo ili kuiwezesha Serikali kupata kanzidata itakayoiwezesha kupanga mipango mbalimbali na kuwawezesha Diaspora kupata fursa zilizopo nchini.


