POLISI WAVAMIA MAKAZI YA RAIS WA ZAMANI WA ZAMBIA KUNASA MAGARI YALIYOIBWA NA MKE WAKE.

MUUNGANO   MEDIA
0


Makumi ya maafisa wa polisi wenye silaha wamevamia makazi ya rais wa zamani wa Zambia Edgar Lungu na kuondoka na magari ambayo inadaiwa yaliibwa na mke wa rais huyo wa zamani.

Katika operesheni hiyo iliyotekelezwa jana Jumatano Polisi walisema wameanzisha uchunguzi kufuatia ripoti ya wizi wa magari matatu na kufanikiwa kuzipata mali hizo katika makazi ya Bi Esther Lungu katika kitongoji cha jiji kuu, Lusaka.

Msemaji wa Polisi Danny Mwale amesema, mshukiwa huyo aliitwa kufika mbele ya polisi jana hiyohiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi ya Zambia, mke huyo wa rais wa zamani anadaiwa "kunyakua" magari hayo, ambayo ni lori aina ya Mitsubishi, na sedan mbili ndogo za Toyota, kwa mwanamke mmoja mwezi Agosti mwaka jana.

Taarifa hiyo ya polisi imeeleza kuwa, mwanamke huyo aliyenyang'anywa magari hayo alilazimishwa kuyasalimisha baada ya kuendeshwa hadi kwenye makazi ya mke wa rais wa zamani.

Rais Hichilema (kulia) na Lungu

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, wafuasi kadhaa wa Lungu hasa kutoka chama tawala cha zamani cha Patriotic Front walifika mbele ya nyumba yake kuonyesha mshikamano kwa rais huyo wa zamani wa Zambia na familia yake.

Katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2021, Edgar Lungu alishindwa na rais wa sasa Hakainde Hichilema, ambaye kabla ya kushinda kura kwa kishindo alikuwa kiongozi mkongwe wa upinzani.

Wakati operesheni ya upekuzi na uondoaji magari hayo yanayodaiwa kuibwa na mke wa Lungu ilipokuwa ikiendelea hapo jana, msemaji wa chama chake Raphael Nakachinda, aliituhumu serikali ya Hichilema kwa kile alichokiita "kichaa sugu na hasira za kulipiza kisasi".

Chanzo #Parstoday.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)