Na Emmanuel Kawau.
Makandarasi nchini wametakiwa kuzingatia viwango vya ubora katika ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuongeza tija ya miradi husika na kupiga hatua za kimaendeleo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi Naibu Waziri wa ujenzi na uchukuzi anayesimamia sekta ya ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi chini ya kiwango na rushwa kunashusha thamani ya wakandarasi.
Aidha Kasekenya amewataka Makandarasi nchini kuungana pale inapotokea tenda za miradi mikubwa ili kupata nguvu ya pamoja na kuomba tenda hizo ndani na nje ya nchi na kuzitekeleza kwa pamoja,na ukizingatia kuwa wakandarai wengi hawana uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa peke yao.
"Tunategemea kupitia wataalamu wetu tuungane na kuweza kufanyakazi katika miradi mikubwa sio Tanzania pekee bali hata kwa tenda zinazotangazwa nje ya nchi".
Kadhalika amesisitiza kuwa Serikali itahakikisha malipo kwa Makandarasi yanafanyika kwa wakati,kwa kuwa Ucheleweshaji huo si tu unatoa changamoto kwa wakandarasi pia unachelewesha huduma za maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili Makandarasi (CRB) Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema sekta ya Makandarasi inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa kazi hususani wa majengo na hali hiyo inatokana maamuzi ya Serikali kutumia mfumo wa Force account.
Pia ameitaja changamoto nyingine ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya manunuzi ya umma na kanuni zake ikiwemo Advance payment na dhaman za zabuni ambapo inaleta changamoto kubwa katika utekezaji wa ujenzi.
