RC ALBERT CHALAMILA AMPONGEZA RAIS SAMIA NA WIZARA YA AFYA KWA MAPAMBANO YA UGONJWA WA MARBURG.

MUUNGANO   MEDIA
0

Katika kuhakikisha elimu ya ugonjwa wa Marburg inafika kila kona mkoani Kagera leo April, 25,2023 zaidi ya watu 3000 wamefikiwa na elimu ya tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg katika mwalo wa Nyamkaza  Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera kwenye mashindano ya  kupiga Kasia pamoja na kuogelea yaliyokwenda sambamba na uzinduzi wa boti ya  Mv.Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Akizundua boti hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe.Albert Chalamila ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na watalaam wa Afya na wadau wa kitaifa na kimataifa  kwa kujidhatiti katika mapambano ya ugonjwa huo hali iliyosababisha kutokuwepo kwa  maambukizi mapya tangu ugonjwa huo uripotiwe.

“Juzi tumeona hapa na leo nitoe tangazo hili kwa wavuvi wote, kulikuwa na ugonjwa unaitwa Marburg mliusikia,huu ugonjwa kwa mara ya kwanza ulikuja kwa njia ya hawa wavuvi, mgonjwa wa kwanza akafa,wa pili mpaka wa tano, na ule ugonjwa tunamshukuru sana Rais Samia ,Wizara ya Afya na wadau wetu kwa kuchukua hatua za haraka ,na wasingechukua hatua za haraka wangekufa zaidi ya watu 700 lakini nashukuru kwa kuwaambia waliofariki mpaka sasa ni 6 na tuliokuwa tumewaweka karantini wote wamepona ,tunaendelea kuomba Mungu magonjwa kama haya yapotee”amesema.

Aidha,Mhe.Chalamila amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan tayari ameshatoa Tsh.Bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Magonjwa ya mlipuko kinachotajia kugharimu zaidi ya Tsh.bilioni 6 .

Beauty Mwambebule kutoka Wizara ya Afya, akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma,Idara ya Kinga,Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga amesema  amesema kupitia hadhara hiyo imesaidia kuwafikia walengwa namna ya kujinga na magonjwa mbalimbali ya mlipuko ikiwa ni pamoja na Marburg na Kipindupindu.

“Hawa zaidi ya watu tuliowafikia kwa wakati mmoja watakuwa mabalozi namna ya kujilinda dhidi ya magonjwa ya mlipuko  hivyo ni muhimu kila mmoja kuendelea kuzingatia kanuni za afya wakati wote iwe kama desturi yetu kuhakikisha tunanawa mikono mara kwa mara si kwa ajili ya Marburg pekee bali na magonjwa mengine ya mlipuko kama kipindupindu’’amesema Beauty.

Ikumbukwe boti ya Mv.Dkt.Samia Suluhu Hassan ilitolewa na Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kama zawadi kwa Wavuvi ambapo alitoa jumla ya Tsh.milioni 30 huku milioni 15 walifanya maamuzi ya kununua boti hiyo  ya utalii kama sehemu ya mapato na hii ilikuja mara baada ya kutokea ajali ya ndege ya Precision Air na kuona juhudi kubwa za uokoaji zilizofanywa na wavuvi ambapo pia walipatiwa mafunzo namna ya uokoaji  ndani ya maji.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)