WAZIRI DKT MABULA AFAFANUA UPOTOSHAJI VIWANJA VINAVYOMILIKIWA NA KAMPUNI YA SLIPWAY TOWERS LTD.

MUUNGANO   MEDIA
0

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametoa ufafanuzi wa viwanja vinavyomilikiwa kampuni ya Slipway Towers Ltd vilivyopo Msasani Peninsula jijini Dar es Salaam ambapo amemuagiza katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eng. Anthony Sanga kuchunguza kubaini kama kuna wataalam waliohusika katika upotoshaji huo ili waweze kuchukuliwa hatua za haraka za kinidhamu.

Aidha, Dkt Mabula ameelekeza kuwa, kuanzia sasa Manispaa ya Kinondoni inapotaka kupangisha maeneo au eneo ambalo ni kwa matumizi ya umma inatakiwa kijiridhisha kwanza kwa lengo la kujua eneo husika kama mipaka yake haijaingiliana na wapangishaji wengine ili kuepuka migogoro.

Kumbukumbu za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinaonesha kuwa viwanja namba 1497, 1498 na 1856 vinamilikiwa kampuni ya Slipway Towers Limited kwa hati namba 29035 ya muda wa miaka 99 iliyotolewa Januari 1, 1980 kwa ukubwa wa hekta 1.383 kama ilivyo kwenye ramani ya usajili namba 18460 ya mwaka 1980.

Hata hivyo, upimaji wa viwanja ulirejewa na kufanyiwa maboresho yaliyoongeza kiwanja namna 1967 ambapo kampuni ya Slipway Towers Ltd iliomba kiwanja husika kuunganishwa kwenye hati moja na maombi kukubaliwa na kusajiliwa Agosti 13, 1998 ambapo ukubwa uliongezeka kutoka hekta 1.383 hadi 1.8759.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, uhakiki uliofanywa na wataalam wa wizara yake umebaini kuwa, siyo kweli kwamba mwekezaji kampuni ya Slipway Towers Limited imeingia baharini kwa mita 850 bali zilizotajwa ni mita za mraba ambazo Manispaa ya Kinondoni imempangisha kampuni ya Dorishers ndani ya kiwanja cha hati milki namba 29035 kinachomilikiwa na kampuni ya Slipway Towers Limited.

"Tangu mwaka 1998 hadi sasa wizara haijapata maombi ya Slipway kufanya mabadiliko yoyote kwenye ramani au hati miki na hakuna jambo lolote wizarani linalohusiana na upimaji au umilikishaji unaohusina na kampuni ya Slipway towers ltd, kilichosemwa na meya wa manispaa ya kinondoni kuwa kuna mchakato unaoendelea ndani ya wizara hakipo na hakuna mchakato wala maombi". Alisema Waziri Mabula.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)