Dkt. Tumaini Haonga Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya.
Dkt. Issessanda Kaniki Mganga Mkuu Mkoa wa Kagera.
Baadhi ya Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii katika Kata ya Maruku wakijadili namna ya utekelezaji wa utoaji wa elimu ya ugonjwa wa Marburg baada ya kupewa mafunzo wakiwa sambamba na wawakilishi kutoka Wizara ya Afya pamoja na Red Cross Society.
Mmoja wa Wahumu wa Afya ngazi ya Jamii kutoka Kata ya Maruku akionesha namna nzuri ya Unawaji wa mikono baada ya kupata Mafunzo ya kuwajengea uwezo kutoka Wizara ya Afya ,nyuma yake ni watumishi kutoka Red Cross Society .
Baadhi ya Magari ya Matangazo yenye ujumbe usemao "Jikinge na Marburg,Iweke Jamii yako Salama;Mtu ni Afya ,Afya Yangu, Wajibu Wangu, Piga 199 Bure "yaliyofungwa Muziki unaotoa ujumbe wa tahadhari ya Kujikinga na ugonjwa wa Marburg .
Mwakilishi kutoka ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa Jackline Saulo akikabidhi bango la uelimishaji kwa Mkuu wa gereza la Bukoba , pembeni yake ni mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Beauty Mwambebule.
Wawakilishi kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma , ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wakiwa katika picha ya pamoja katika gereza la Bukoba baada ya kutoa elimu ya ugonjwa wa Marburg.
Baadhi ya wananchi Bukoba wakifuatilia kwa makini vipeperushi vya elimu ya ugonjwa wa Marburg .
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Beauty Mwambebule akitoa elimu ya kujikinga ugonjwa wa Marburg katika shule ya Msingi Kilaini.
Katika kukabiliana na Ugonjwa wa Marburg ulioripotiwa rasmi
mnamo tarehe 21 Machi, 2023 mkoani Kagera, Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa
kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara zingine za
Kisekta pamoja na Wadau mbalimbali inaendelea kutekeleza mikakati ya
uelimishaji na uhamasishaji jamii ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo
Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 1,322 katika Mitaa, Vijiji na Vitongoji
vyote vya Halmashauri ya Bukoba Vijijini na Manispaa ya Bukoba.
Hayo yamebainishwa leo April 8, 2023 katika Manispaa ya
Bukoba Mkoani Kagera na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya
kwa Umma ,Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga wakati akizungumza katika
mwendelezo wa utoaji wa elimu ya afya kuhusu kinga na tahadhari dhidi ya
Ugonjwa huo.
“Kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Serikali
imetekeleza mikakati mbalimbali ili kuzuia ugonjwa huu usienee maeneo mengine
nchini. Ili kuwafikia wananchi mahali ambapo wanapatikana, Serikali
inawatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwa kuwajengea uwezo wahudumu
wapatao 1322 ambapo kati yao Wahudumu wanatoka Halmashauri ya Manispaa ya
Bukoba na Wahudumu wanaobaki wanatoka katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini”
amesema.
Dkt. Haonga amesema sambamba na kuwatumia Wahudumu wa Afya
ngazi ya Jamii katika kutoa elimu ya afya katika maeneo mbalimbali, Serikali
pia imetoa magari 8 maalum ya matangazo kwa ajili ya utoaji wa elimu ya Ugonjwa
wa Marburg katika maeneo mbalimbali hususan sehemu zenye mikusanyiko.
“Utoaji wa magari haya 8 ni kuweka wigo mpana zaidi wa
kuelimisha na kuhamasisha wananchi kupata uelewa na kuzingatia njia za
tahadhari dhidi ya ugonjwa huu”amesema Dkt. Haonga.
“Kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani
(UNICEF), Shirika la Tanzania Interfaith Partneship (TIP) na Uongozi wa
Mkoa tumeweza kuwafikia viongozi wa dini 310 kwa ajili ya kuwajengea
uwezo sambamba na hilo tunaendelea kutoa vielelezo vya elimu kuhusu ugonjwa wa
Marburg” amesema.
Katika uelimishaji kwa Taasisi za Umma Dkt. Haonga
karibu shule zote zimeweza kufikiwa pamoja Taasisi zingine ikiwemo magereza,
sehemu za Ulinzi na Usalama ikiwemo jeshini na vielelezo vyote vya kutolea
elimu vimekuwa vikitolewa kwenye taasisi hizo ambapo Chama cha Msalaba Mwekundu
Tanzania (Tanzania Red Cross Society) kimekuwa kikishirikiana na Wizara ya Afya
katika utoaji wa elimu ya afya kwa umma.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Mkoa wa Kagera Dkt.
Issessanda Kaniki amesema baada ya kuunganisha nguvu kwa Wizara ya Afya,
Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Majanga, Wizara
ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Wadau pamekuwa na matokeo chanya katika suala
la uelimishaji.
“Baada ya kuunganisha nguvu kupitia Wizara yetu ya Afya
,Wizara zingine za Kisekta pamoja na wadau mbalimbali mwitikio ni mkubwa ,watoa
huduma ngazi ya jamii kwa kushirikiana na Tanzania Red Cross Society (TRCS) wameendelea
kufikia jamii katika maeneo tofauti, hivyo nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi
wa Kagera waendelee kutoa ushirikiano kwa kuzingatia njiq za kinga na tahadhari
zinazoshauriwa kitaalamu”amesema.
Naye Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa
Uhamiaji, Thomas Fussy amesema wataendelea kushirikiana na jitihada
zinazofanywa na Wizara ya Afya za kuhakikisha wageni wote wanaowahudumia
wanazingatia kanuni za afya ikiwemo kuhamasisha wananchi kunawa mikono
mara kwa mara.
“Mkoa wa Kagera una mipaka saba, kupitia elimu tuliyopewa na
Wizara ya Afya kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, tutaisambaza katika
sehemu mbalimbali tunazotoa huduma ikiwa ni pamoja na sehemu za mipakani hivyo
tunaipongeza sana Wizara ya Afya kwa kujidhatiti katika kutoa elimu kila mahali
“amesema.
MWISHO.
