Albert Chalamila Mkuu wa Mkoa wa Kagera akizungumza katika kikao cha kamati ya Wajumbe Maalum wa kukabiliana na Ugonjwa wa Marburg kilichofanyika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Dkt.Issesanda Kaniki Mganga Mkuu Mkoa wa Kagera akizungumza katika kikao cha kamati ya Wajumbe Maalum wa kukabiliana na Ugonjwa wa Marburg kilichofanyika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Wajumbe Maalum wa kukabiliana na Ugonjwa wa Marburg kilichofanyika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe.Albert Chalamila ameipongeza Timu ya Watalaam wa Afya kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum ,Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa pamoja na wadau kutoka mashirika mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa kwa kuendelea kushirikiana na Mkoa katika Mapambano ya Ugonjwa wa Marburg.
Mhe.Chalamila ametoa pongezi hizo leo April, 10, 2023 katika kikao cha kamati ya Wajumbe Maalum wa kukabiliana na Ugonjwa wa Marburg kilichofanyika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Mhe.Chalamila amesema kazi inayofanywa na kamati hiyo ni kubwa sana katika kukabiliana na ugonjwa wa Marburg .
“ Nitumie nafasi hii kuwapongeza kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya, na ninyi kutoka mashirika ya Kimataifa mmetusaidia sana kufikisha ujumbe uliosahihi na taswira ya nchi yetu kwa mataifa mbalimbali na ninachosisitiza ninyi wataalam wa afya lazima muwe na ujasiri wa kitaaluma”amesema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dkt.Issesanda Kaniki ametoa shukrani na pongezi kwa Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwa kuchukua hatua za haraka ikiwemo kutuma timu ya madaktari bingwa 12 wameweka kambi mkoani Kagera mara tu ugonjwa wa Marburg uliporipotiwa.
“ Kama tunavyofahamu ugonjwa huu unakimbilia kwenye viungo muhimu kama figo kutofanya kazi, tulikumbana na changamoto ambapo ilibidi tuwe na madaktari bingwa kwa jitihada za Mkoa kwa kushirikiana na Waziri wa Afya tuliweza kupata madaktari bingwa 12”amesema.
Aidha, Dkt. Kaniki amesema jumla ya watu 212 waliotangamana na wagonjwa wamefuatiliwa ,kati yao watu 174 wamekamilisha siku 21 za uangalizi hadi kufikia April, 8,2023.
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Epidemiolojia na udhibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vida Mmbaga amesema wanafanya mahojiano na watu mbalimbali ikiwemo watu mashuhuri kwa ajili ya kufanikisha kupata taarifa kwa kuwepo kwa mgonjwa katika maeneo husika.
MWISHO






