Mmoja kati ya wagonjwa watatu waliokuwa wamelazwa kutokana na ugonjwa wa Marburg aitwae Bw. Mushobozi Washington mkazi wa kata ya Kanyengereko Wilaya ya Bukoba vijijini mkoani Kagera amepona na kuruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Bujunangoma.
Akiongea na wanahabari leo Bw. Mushobozi amesema mnamo Tarehe 15 Machi 2023 alipata dalili ambazo ziligundulika kuwa ni za ugonjwa wa Marburg baada ya kwenda hospitali na kufanyiwa vipimo.
"Nilikuwa na tapika na kupelekwa katika hospitali ya Maruku ambapo nilibainika kuwa na ugonjwa wa Marburg nikawa naendelea na matibabu na baadae nikapelekwa Hospitali ya Wilaya Bukoba Vijijini ya Bujunangoma ambapo mpaka sasa najiskia vizuri na nimeruhusiwa kurudi nyumbani".
Kwa furaha Bw. Mushobozi ameishukuru Serikali na watoa huduma wa kituoni hapo kwa kumuhudumia kwa usahihi muda wote alipokuwa kituoni hapo na kuakikisha wanaokoa maisha yake.
Pia Bw. Mushobozi amewashauri wananchi wote wakipata dalili za ugonjwa wowote wasikimbilie mtaani wafike kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakapatiwe huduma.
Nae Dkt. Noel Saitoti kwa niaba ya watoa huduma waliokuwa wanamuhudumia Bw. Mushobozi amewataka wananchi wa kijijini kwake kumpokea vizuri na kuto mnyanyapaa kwani amepona kabisa na hivyo kutoweza kuambukiza wengine.