WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, MHE. DKT. STERGOMENA TAX AKIZUNGUMZA NA WAJUMBE WA KAMATI YA KUTATHMINI UTENDAJI WA WIZARA YA MAMBO YA NJE WALIPOKUTANA NAYE OFISINI KWAKE JIJINI DODOMA TAREHE 18 APRILI 2023 KUASHIRIA KUANZA RASMI KWA KAZI YA KAMATI HIYO. KAMATI HIYO YENYE WAJUMBE 7 INAONGOZWA NA BALOZI MSTAAFU, MHE. HASSAN SIMBA YAHYA (WA KWANZA KUSHOTO).
Kamati iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutathimini utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeanza kazi rasmi kwa kukutana na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax jijini Dodoma leo tarehe 18 Aprili 2023.
Wakati wa kikao hicho, Mhe. Dkt. Tax aliwapongeza wajumbe wa kamati hiyo kwa kuaminiwa na Mhe.Rais Samia na aliwaahidi kuwa Wizara itatoa ushirikiano unaohitajika ili Kamati hiyo iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Hii ni Kamati muhimu sana na ni matumaini ya Mhe.Rais Samia kuwa mtafanya kazi nzuri itakayoleta mapendekezo yatakayoboresha utendaji wa Wizara ili kukidhi malengo ya Serikali ya kukuza diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa Kimataifa” Mhe. Dkt.Tax aliwambia wajumbe wa kamati hiyo.
Mhe. Dkt. Tax alisema wajumbe wa Kamati hiyo takribani wote ni wenyeji wa Wizara ya Mambo ya Nje na wabobevu katika masuala ya diplomasia, hivyo ana uhakika kwa muda waliopewa na hadidi za rejea walizopewa, watafanya kazi itakayokidhi matarajio ya Mhe. Rais Samia.
Kamati hiyo ina wajumbe 7 ambao ni mabalozi wastaafu; Mhe.Hassan Simba Yahya, (Mwenyekiti), Mhe. Ramadhani Muombwa Mwinyi (Mjumbe); Mhe. Mwanaidi Sinare Maajar (Mjumbe); Mhe. Peter Allan Kallaghe (Mjumbe); Mhe. Tuvako Nathaniel Manongi (Mjumbe); Mhe. Jack Mugendi Zoka (Mjumbe); na Mhe. George Kahema Madafa (Mjumbe).
Kamati hiyo iliundwa na Mhe. Rais Samia tarehe 28 Machi 2023.