.
Lango kuu la Gereza la Bukoba Mkoani Kagera. 
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Beauty Mwambebule akitoa elimu jinsi ya kujikinga na Marburg katika gereza la Bukoba mkoani Kagera.
Mmoja wa Maaskari magereza ,gereza la Bukoba akizingatia kanuni za afya kwa kunawa mikono kwa maji tiririka .Mtaalam wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Jackline Saulo
Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Jumla ya watu 805 wakiwemo wafungwa, watumishi wa magereza pamoja na
familia zao katika Gereza la Bukoba Mkoani Kagera wamefikiwa
na elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa Marburg .
Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Dkt.Tumaini Haonga baada ya kutembelea gerezani hapo kutoa elimu namna ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg, Beauty Mwambebule amesema Marburg ni muhimu kuchukua tahadhari mapema juu ya ugonjwa huo.
“Kinga ni bora kuliko tiba ; wakati mwingine inaweza kuchukua kuanzia
siku 2 hadi 21 kuonesha dalili mfano homa, kutapika, kuharisha damu au kutapika
damu ni muhimu tuchukue tahadhari mapema” amesema Beauty Mwambebule, Mwakilishi
wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya.
Kwa upande wake Mtaalam wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Jackline Saulo amesema ni muhimu kwa kila mtu kuepuka misongamano isiyo
ya lazima ambapo pia maelekezo yameshatolewa kuhakikisha sehemu zote zenye
mikusanyiko ya watu panakuwepo na vifaa maalum vya kunawia mikono.
Wakitoa neno la shukrani baadhi ya watumishi wa Gereza la Bukoba akiwemo
Mkaguzi wa Jeshi la Magereza Fredrck Katabazi huku Mkaguzi Msaidizi
Venance Vedastus ambaye ni afisa mapokezi gereza la Bukoba
wametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kuwa mstari wa mbele katika
kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mara tu yanaporipotiwa hasa kwa kuongeza
wigo wa uelimishaji.
Pia katika gereza la Bukoba yametolewa mabango yenye ujumbe mahsusi kuhusu
elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa Marburg , dalili zake na jinsi unavyoenezwa.
Ikumbuke kuwa watalaam wa Afya kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na
Mkoa wa Kagera wameendelea kutoa elimu jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg
katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera kwa kufikia makundi mbalimbali
ikiwemo magereza, viongozi wa dini, waendesha pikipiki, maduka na sehemu zote
za kutolea huduma na sehemu zenye mikusanyiko.
MWISHO.




