ZAIDI YA WATOTO 40,000 WAPATIWA CHANJO MPIMBWE KWA USHIRIKIANO WA WAGANGA WA TIBA ASILIA

MUUNGANO   MEDIA
0

Na Mary Baiskeli, Katavi.

Waganga wa tiba asilia katika halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele waliosababisha kushamiri ugonjwa wa surua na kuiathiri jamii, kutokana na wazazi kuendekeza imani za kishirikina kwasasa wamebadilika na kuwezesha watoto zaidi ya 40,000 kuchanjwa.

Akizungumza katika halaiki ya wananchi wa halmashauri ya Mpimbwe katika kongamano la kumpongeza rais kuboresha huduma za kijamii Mkuu wa wilaya ya Mlele Majid Mwanga amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wao.

 “Lengo lilikuwa kuchanja watoto thelathini na tisa elfu katika halmashauri ya Mpimbwe kutokana na kata ya Majimoto kuathirika zaidi na surua,”

“Nafurahi kuwaeleza kuwa zaidi ya watoto arobaini na nne elfu wamepata chanjo hiyo katika halmashauri ya Mpimbwe,”

Mafanikio hayo yamepatikana baada ya serikali ya wilaya kuwaomba waganga wa jadi wawatibu wagonjwa wao baada ya kumalizana nao wawapelekee watoa huduma za afya.

“Watu wengi wanakwenda kwa wenzetu kupata huduma usiku, nawaomba pamoja na kutibiwa kwa njia za asili jengeni utamaduni wa kupata matibabu ya kitaalamu ili kunusuru afya zenu na watoto,”

“Tukifanya hivyo ugonjwa wa surua hauwezi kuiathiri tena Mpimbwe,badilikeni ndugu zangu kwasababu serikali ipo kwaajili yenu,”amesema Mwanga.

Mbali na hilo amewaeleza wananchi kuwa serikali wilayani Mlele kupitia uongozi wa awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imepokea zaidi ya sh.196.6 bilioni kutekeleza miradi ya afya, elimu, maji, barabara na miundombinu ya umeme.

 “Wale mnaosafiri na barabara ya kwenda Tabora mmeona nguzo nyingi zimewekwa, hayo ndo matamanio ya rais ya kuachana na umeme wa jenereta na mafuta tuingie kwenye gridi ya taifa,”

Amesema umeme huo utakapofika Mpimbwe utasaidia viwanda vinavyofanya kazi kwa kutojiamini vitaweza kuzalisha zaidi.

Shigela John mmoja wa waganga wa tiba asilia amesema wametambua wajibu wao wa kutoa hamasa kwa wagonjwa wao kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

“Tumewahamasisha wazazi kuwapeleka kwenye chanjo wamejitokeza kwa wingi,tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali,”amesema Shigela.

Naye Anjeli Mwakalinga amesema wanamshukru rais kwa juhudi anazofanya kwa kuwa ameboresha huduma za kijamii tofauti na ilivyokuwa awali.

“Ni muda mfupi tangu aingie madarakani ameboresha shule,barabara, afya, maji na mengine hatuna tatizo naye aendelee kufanya kazi ,”

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)