Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera , Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene amezitaka Wizara za Kisekta kuwa na nguvu ya pamoja katika kukabiliana na kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu hapa nchini.
Aidha, Waziri Simbachawene ameziagiza Halmashauri na Mikoa zote nchini kutoa elimu kwa wananchi kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya Maji kwa kuoga, kufua, na kutupa takataka ovyo.
Waziri Simbachawene amebainisha hayo leo Machi.22.2023 Jijini Dodoma katika Uzinduzi wa Mpango Shirikishi wa Taifa wa Kuzuia na Kukabiliana na Kipindupindu kwa Kipindi cha miaka minne(2023-2027).
Waziri Simbachawene amesema katika kupunguza madhara ya Mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu ni muhimu wananchi wakapewa elimu Kwa kuzingatia kanuni za afya.
"Ofisi za tawala za mikoa na serikali ni muhimu kutoa elimu kwa wananchi kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji na ni jambo la Msingi Kwa wananchi kuacha kutiririsha maji ya vyoo kwenye mifereji ya wazi." amesema Waziri Simbachawene.
Kuhusu suala la Kinga,Waziri Simbachawene amehimiza zaidi kuweka mkazo wa Afya ya Kinga .
"Tuwakinge wasiugue Ili wasiende hospitalini hivyo natoa wito kwa Wizara ya Afya kuongeza nguvu katika masuala ya elimu na ufuatiliaji wa Magonjwa"amesisitiza Waziri Simbachawene.
Katika hali ya upatikanaji wa maji, Mhe.Simbachawene ameziagiza Ofisi za tawala za mikoa na halmashauri zote kushirikiana na Mamlaka za maji za mjini na vijijini(RUWASA) Ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji unaimarika.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel Kwa niaba ya Waziri Ummy Mwalimu amesema mpango huo utakuwa na tija kubwa katika kukabiliana na Kipindupindu.
Aidha, Dkt. Mollel amesema kuwa kwa mwaka 2015 Tanzania ilikuwa na visa vilivyoripotiwa vya ugonjwa wa kipindupindu 12,985 wakati kwa mwaka wa 2022 visa vilivyoripotiwa ni 537 na upungufu huo ni kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mh Dkt Samia Suluhu Hassan.
Ikumbukwe kuwa Ushirikiano wa Kisekta ni mkakati sahihi wa kuzuia,kukabiliana na kutokomeza Kipindupindu nchini ifikapo 2030.