Na. Majid Abdulkarim, Singida.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya ,Dkt. Grace Magembe amevitaka vituo vyote vya kutolea huduma za afya Mkoani Singida kutoa chanjo kwa Watoto 62,000 waliopo chini ya umri wa miaka Mitano.
Dkt. Grace ametoa kauli hiyo leo katika ziara yake ya Kikazi Mkoani humo na kusema Vituo vyote vinatakiwa kuchanja watoto wote chini ya umri wa miaka mitano katika maeneo yake huku akisisitiza ubora wa huduma katika maeneo ya kutolea huduma za afya.
“Watoto wote waliopo chini ya miaka mitano ambao hawajachanjwa wapatiwe chanjo ili kuepuka magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kuzuilika kwa chanjo” amesema Dkt. Grace.
Aidha amewakumbusha watumishi kuzingatia weledi na viapo vya taaluma zao na utamaduni wa kufanya ukaguzi wa ubora wa huduma na ukaguzi wa vifaa tiba ili kuleta ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi.
“Mkifanya ukaguzi wa ndani na ubora wa huduma mtaleta ufanisi katika utendaji kazi wenu na wananchi watafurahia huduma zenu “.
Pia, Dkt. Grace amewataka kuwa na mpango mkakati wa matengenezo ya vifaa tiba katika hospitali wanazofanyia kazi lakini pia kuzingatia usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma ili kuepuka magonjwa.
''Tunawajibu wa kuwalinda watumishi na wagonjwa tunao wahudumia wasipate magonjwa na kuhakikisha tuko salama ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi, kutobeba maradhi kwa familia zao, kuwa na maji tiririka katika vituo vya afya”, amesema Dkt. Grace.
Watumishi wa afya wametakiwa kujiepusha na rushwa katika vituo vyetu vya kazi ili kuleta utendaji mzuri wa kazi vituoni.Hata hivyo amehitimisha na kuwakumbusha watumishi kufanya kazi kwa weledi na bidii kulingana na majukumu wanayopaswa kufanya ili kuongeza ufanisi katika sekta ya Afya.