RC DODOMA APOKEA TUZO YA RAIS SAMIA NI KATIKA MASUALA YA MAENDELEO YA ELIMU.

MUUNGANO   MEDIA
0

TAASISI ya Professor Mwera Foundation ya mkoani Mara inayojishughulisha na masuala ya elimu imempa tuzo Rais Dr. Samia Suluhu Hassan kutokana na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mh. Rosemary Senyamule na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Hezbon Mwera Machi 30, 2023 katika mkutano wa wadau wa sekta ya elimu Mkoani Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Prof. Mwera,Mkurugenzi wa Taasisi hiyo,Hezbon Mwera amesema kwa kutambua jitihada na mchango katika sekta ya elimu unaotolewa na Rais Samia wameamua kumpa tuzo hiyo ya heshima.

Amesema Taasisi hiyo inajishughulisha na mambo ya kijamii na wamepewa kibali na ofisi ya Tamisemi kufanya shughuli zao ndani ya Mikoa 10 ya Tanzania.

Amesema shughuli wanazozifanya ni pamoja na kuhamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi kwani kila mmoja anajua umuhimu wa vijana kupata mafunzo ya Elimu ya ufundi baada ya kumaliza darasa la saba na kidato cha nne wakati wakisubiri matokeo.

"Nipende kumpongeza Rais Samia kwa kuanzisha vyuo katika kila Wilaya.Taasisi yetu hii pia inashirikiana na Ofisi za Mikoa kutoa tuzo kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya darasa la saba, kidato Cha nne na sita,"amesema.

Mkurugenzi huyo wa Taasisi hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, amesema wametoa tuzo katika Mikoa ya Mwanza,Kigoma,Simiyu,Shinyanga,Geita ,Mara.

Pia alimkabidhi tuzo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule kwa kumpongeza yeye pamoja na wasaidizi wake katika kuongeza ufaulu mkoani humo.

Tuzo za jumla zilizotolewa katika hafla hiyo zilidhaminiwa na taasisi ya ya Professor Mwera Foundation ya mkoani Mara.

Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mh. Rosemary Senyamule,ameipongeza taasisi hiyo kwa kazi nzuri inazofanya katika sekta ya elimu kwenye mikoa mbalimbali nchini.

RC Senyamule amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanya jitihada kubwa kuhakikisha watoto wote wanaenda shuleni na matarajio ya Serikali ya awamu ya sita ni kuona elimu bora inatolewa pamoja na changamoto zote zinatatuliwa.

"Ili Mkoa uweze kusonga mbele kielimu ni lazima tuhakikishe watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na wanahudhuria shule wakati wote,"amesema Mkuu huyo wa Mkoa.

Mkuu huyo wa Mkoa ameupongeza Mkoa huo kwa kushika nafasi ya 10 kitaifa kwa matokeo ya mwaka 2022.

"Niendelee kusisitiza yale tutakayokubaliana tukayatekeleze,niwaombe tuzidi kupambana kuhakikisha tunafanya vizuri,"amesema Mkuu huyo wa Mkoa.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)