Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la ofisi yake kuainisha na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zitakazokwamisha utekelezaji wa bajeti ya ofisi ya Mwaka wa Fedha 2023/24 inayotarajiwa kuidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi na Utawala Bora kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Bw. Mkomi ametoa maelekeo hayo jijini Dodoma, wakati akiongoza Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililofanyika kwa lengo la kupitia Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2022/23 na Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2023/24.
Bw. Mkomi amesema kila mwaka Bunge linaidhinisha bajeti lakini wakati wa tathmini mapungufu yanabainika katika utekelezaji, hivyo aliwasihi wajumbe wa baraza kutumia fursa ya mkutano huo kuainisha na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24.
“Ni wajibu wa kila mjumbe wa baraza hili kutoa mapendekezo yatakayowezesha utekelezaji wa bajeti yetu kwa mwaka wa fedha 2023/24 pindi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litakapoidhinisha” Bw. Mkomi amesisitiza.
Aidha, Bw. Mkomi amesema, ushirikiano wa kiutendaji chini ya uongozi wake ni suala analolipa kipaumbele ili kufikia azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuujenga utumishi wa umma unaowajibika kwa wananchi katika kutoa huduma bora.
Bw. Mkomi ametoa wito kwa wajumbe wa mkutano huo maalum kumshirikisha iwapo wana wazo au jambo ambalo wanafikiri likitekelezwa litakuwa na tija katika kuuboresha utumishi wa umma.
Bw. Mkomi ameongeza kuwa, suluhu ya kuboresha utendaji kazi wa watumishi wasiowajibika si kuwahamisha vituo vya kazi bali waajiri wahakikishe wanarekebisha mapungufu yao ili waendelee kutoa huduma katika vituo vyao vya kazi walivyopangiwa.


