Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kusini, ipo katika zoezi la ukaguzi na utoaji wa elimu katika Hospitali, Vituo vya Afya, Zahanati na maduka ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi (Binadamu na Mifugo) katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara kwa wiki hii.
Zoezi hilo linaongozwa na Dkt. Engelbert B. Mbekenga, Meneja wa TMDA Kanda ya Kusini, akielezea umuhimu wa zoezi hilo, Meneja amesema ni sehemu ya majukumu ya Mamlaka katika kazi zake za kila mwaka katika kutekeleza majukumu yake, lengo ni kuhakikisha katika jamii kuna kuwa na dawa, vifaa tiba na vitendanishi vilivyo salama, bora na ufanisi.
Meneja, Dkt. Engelbert B. Mbekenga amesema kuna watoa huduma wasio na sifa, uuzaji holela wa dawa katika maduka ya dawa muhimu hivyo basi ukaguzi huu upelekea kuondoa changamoto hizo katika maeneo hayo. Pamoja na ukaguzi imekuwa ikitoa elimu kwa wamiliki na wauzaji kwa lengo la kupata uelewa wa dawa aina gani zinaruhusiwa na umuhimu wa kuwepo kwa watoa huduma wenye sifa katika kutoa huduma katika maduka ya dawa muhimu.
Meneja amesema ukaguzi ubaini matendo maovu ya watoa huduma na muda mwengine wamiliki wanachangia kwa nia ya kutaka kupata faida kama kutoa huduma ya kuchoma sindano, kuuza dawa zisizotakiwa katika ngazi ya maduka ya dawa muhimu.
Zoezi la ukaguzi na elimu kwa ngazi ya Hospitali, vituo vya Afya, Zahanati na maduka ya dawa ni endelevu kwa wiki hii yote kwa upande wa Newala Mji na Halmashauri ya Newala, wamewaomba wamiliki na watoa huduma kutoa ushirikiano wakati wote wa ukaguzi, Ukaguzi ni njia ya kuboresha huduma katika sekta ya afya.
Afisa Elimu kwa Umma na Huduma kwa Wateja, TMDA Kanda ya Kusini, Bw. Hussein Makame, ameongezea zoezi la elimu kwa jamii juu ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi ni muhimu na limekuwa likitekelezwa kwa uweledi mkubwa sana na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba -TMDA katika ofisi zake zote nchini.