TBPL YATAKIWA KUJITANGAZA NDANI NA NJE YA NCHI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji (Mb.) amekitaka Kiwanda cha Serikali cha kuua viuadudu na viluwiluwi vya mbu (TBPL) kujitangaza ndani na nje ya nchi ili kuongeza wigo wa masoko kwa kuuza bidhaa hiyo ya kipekee inayozalishwa hapa nchini.

Dk. Kijaji ameyasema hayo Machi, 29, 2023 alipotembelea kiwanda hicho kilichoko Kibaha Mkoani Pwani kushuhudia namna uzalishaji wa dawa za viuadudu unavyofanyika kiwandani hapo.

“ Serikali imetimiza wajibu wake wa kuwekeza ili kuondokana na suala la Malaria hapa nchini na wajibu wetu ni kuhakikisha tunatoa elimu ya kutosha juu ya matumizi ya dawa hii kwa ajili ya kuua viluwiluwi vya Malaria ili kutimiza adhima ya Serikali". Alisitiza Dkt. Kijaji.

Aidha, Waziri Kijaji ameiagiza TBPL kushirikiana na TANTRADE katika kuhakikisha dawa hizo zinatangazwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kuwa na mipango mikakati ya masoko itakayofanikisha utoaji wa elimu juu ya matumizi ya dawa hizo na faida zake kufika kwa watanzania wengi.

Awali akimkaribisha Mheshimiwa Waziri, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambayo ndio mmiliki wa kiwanda hicho Bw. Alfred Mapunda amesema NDC kwa kushirikiana TBPL wameanza utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kimasoko ikiwemo ukamilishaji wa mkataba wa mauzo baina ya NDC na Wizara ya Afya , pamoja na kuanza mchakato wa upatikanaji wa mawakala wa kuuza na kusambaza dawa hizo katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Katika hatua nyingine Mapunda pia alibainisha juu ya nia ya kiwanda hicho kuanza rasmi uzalishaji wa viuatilifu vya mazao ili kupambana na wadudu waharibifu wa mazao ambapo dawa hizo mara baada ya kufanyiwa majaribio zimeonyesha mafanikio makubwa katika kupambana na wadudu hao hatari kwa ustawi wa sekta ya kilimo hapa nchini.

Akibainisha mafanikio ya kiwanda hicho Mapunda, amesema kimesaidia kwa kiwango kikubwa kushusha kiwango cha Malaria hapa nchini mathalani visiwani Zanzibar ambapo kiwango cha maambukizi ya Malaria kimeshuka hadi sasa kipo chini ya asilimia moja, pamoja na upatikanaji wa masoko ya nchi za nje mathalani katika nchi za Msumbiji, Niger, Eswatin pamoja na Angola.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)