Na Gideon Gregory, Dodoma.
Shirika Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limefanikiwa kuimarisha Usimamiaji na utoaji wa vyeti vya Mabaharia kwa kuzingatia matakwa ya Shirika la Bahari Duniani (IMO) chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Mafunzo, utoaji vyeti na Ufanyaji kazi kwa Mabaharia 1978 ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya vyeti 16,718 vilitolewa.
Hayo yamebainishwa leo Machi 7,2023, na Mkurugenzi mkuu wa Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge wakati akizungumza na wandishi wa habari, amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2022 mpaka Januari 2023, Shirika hilo liliweza kutoa vyeti 9,570 na takribani vyeti 17,000 vinavyotarajiwa kutolewa ifikapo Juni mwaka huu.
Bw. Mkeyenge ameongeza kuwa vilevile wamefanikiwa kimarisha udhibiti wa usalama na ulinzi kwenye maeneo ya shughuli za bandari kwa kusimamia urasimishaji wa maeneo 20 ya kibandari katika mwambao wa bahari na maziwa kama Somanga-Lindi; Kunduchi-Dar es Salaam; Kilongwe-Mafia; pamoja na Nyamisati-Pwani.
“Tumefanikiwa kuongeza mchango katika Mfuko Mkuu wa Serikali mwaka hadi mwaka kutoka Shilingi Bilioni 9.1 katika mwaka wa fedha 2018/19 hadi kufikia Shilingi Bilioni 43.5 katika mwaka wa fedha 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 21 na hivyo kufanya jumla ya mchango wa TASAC katika mfuko mkuu wa Serikali kwa kipindi cha miaka minne kuwa Shilingi Bilioni 104.5”,amesema.
Amesema TASAC pia imehusika kuiwakilisha nchi katika mazungumzo ya muda mrefu na hatimaye kutimia baada ya nchi wanachama wa UN kuafikiana juu ya vipengele muhimu katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya Bioanuwai za Nje ya Mipaka ya Nje ya Kisheria juu ya kutunza Bahari kuu na mazalia yake kwa maendeleo endelevu juzi mjini New York.
“Mbali na Mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho lakini pia kuna fursa mbalimbali katika Sekta ya Usafiri Majini ambazo zinaweza kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi kama vile, kuanzisha utaratibu wa kusajili meli kwa masharti nafuu (open registry), kuanzisha maeneo ya ukarabati na ujenzi wa meli katika ukanda wa pwani, kuanzisha maegesho ya boti ndogo katika ukanda wa pwani, kuanzisha viwanda vya utengenezaji malighafi za ujenzi wa boti za plastiki (fibre) pamoja na kujenga bandari rasmi za uvuvi,”amesema.
TASAC ilianzishwa chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake tarehe 23 Februari, 2018.
Ikumbukwe kuwa kuundwa kwa shirika hilo ni hatua ya kisera ya Serikali, kwa upande wa Tanzania Bara, inayokusudia kukuza sekta za usafiri majini, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hususani kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuinua mchango wa usafiri kwa njia ya maji.

