SEKTA YA MIFUGO IKIIMARISHWA INAWEZA KUWA SEKTA YA KIMKAKATI KATIKA KUKUZA UCHUMI WA NCHI - RC SENYAMULE.

MUUNGANO   MEDIA
0


Na Gideon Gregory, Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule amesema kuwa Sekta ya Mifugo ikiimarishwa inaweza kuwa Sekta ya kimkakati katika kukuza uchumi wa nchi.

Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo Machi 14,2023 Jijini Dodoma katika ziara yake alipotembelea Kampuni ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO), iliyoko wilayani Kongwa ambapo amesema Ranchi hiyo ni sehemu ambayo Serikali imeweka nguvu ili kuhakikisha sekta ya Mifugo inaongeza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa.

“Mara nyingi tumekuwa tukisikia kuwa zipo nchi nyingi za Afrika zinazotegemea Mifugo na hasa ng'ombe na mimi kwa masikio yangu nimekuwa kusikia Ethiopia ndiyo nchi inayouza mifugo mingi nje kuliko nchi yoyote ya Afrika na Tanzania tunasemekana kwa wingi wa mifugo sisi ni wapili hasa ya ng'ombe baada ya Ethiopia,”amesema.


Aidha ameongeza kuwa chanzo cha Tanzania kushika nafasi hiyo ni kutokana na wafugaji wengi wanafuga kienyeji lakini yapo mashamba mengi kama NARCO na wapo wataalamu ambao wamepewa mifugo ili kuonyesha namna ya kufuga kisasa.

Amesema matarajio ya serikali kuputia NARCO ni kutoa ng'ombe wa kisasa kama ni wa nyama, na kama ni wa maziwa yaonekane ni mengi kwa walio tunzwa kisasa na watu wengine wajifunze kutoka katika maeneo hayo ya mashamba na wao wajifunze kufuga kwa kutotembeza mifugo yao na utaalamu mwingine utakao patikana.

Sanjari na hayo amebainisha mikakati ambayo mkoa umeweka ni kifanya mkoa huo kuwa wa utalii ambapo amesema wakitaja vivutio vya utalii vilivyopo ni pamoja na eneo la ukombozi wa Uhuru na NARCO.

“Wengi wanajiuliza mbona NARCO ipo huku hatuioni, tukiingia tutaona utalii gani?, Tunawaambia tunataka tuanzishe sehemu hapo barabarani sehemu ya nyama choma ya kisasa, lakini watu wengi sana wangetamani matumizi ya hawa ng'ombe walioko NARCO ni pamoja na wapita njia walipo katika barabara yetu huenda ingekuwa nafasi kubwa sana ya kuonyesha tofauti ya nyama inayofugwa mtaani na hii inayofugwa NARCO kwa kuweka hapo barabarani,”amebainisha.

Naye Meneja wa Ranchi hiyo Bw. Elisa Binamungu amebainisha dhumuni la kuanzishwa kwake kuwa ni kuendeleza na kueneza ufugaji bora, husasi ufugaji wa ng'ombe bora wa nyama kwaajili ya soko la ndani na nje kwa kutumia mbinu za ufugaji wa kisasa.

Pia ameongeza kuwa changamoto kubwa ambazo wanakabiliana nazo ni pamoja na kiangazi kikubwa kinachoambatana na uchomaji moto, u amizi kwaajili ya kuchoma mkaa na kilimo pamoja na wizi wa mifugo.

Kampuni ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO), ilianzishwa mwaka 1948 chini ya Kampuni ya kiingereza iliyojukana kama Overseas Food Corporation (OFC) kama mradi wa kulima karanga kisha mwaka 1958 kubadirshwa na kuwa na ufugaji wa ng'ombe wa nyama baadala ya kuona hali ya hewa sio nzuri kwa kilimo ukahamishiwa Tanganyika Agriculture Company (TAC) na baada ya Uhuru ukamishiwa National Agriculture Company (NACO), baadae kubadilishwa na kuwa National Ranching Company (NARCO) mwaka 1968 na Kongwa ndiyo waanzilishi.
Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)