PIC YARIDHISHWA UJENZI DARAJA LA JP MAGUFULI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mhe. Jerry Silaa amesema kamati yake inaridhishwa na kasi ya ujenzi wa daraja la JPMagufuli maarufu Kigongo-Busisi lenye urefu wa kilometa tatu na barabara unganishi kilometa 1.66.

Mhe. Silaa amesema uwekezaji katika daraja hilo ni uwekezaji sahihi kwani litafungua huduma za uchukuzi kati ya Kenya, Tanzania na Uganda kupitia Sirari-Musoma-Mwanza-Geita,Bukoba hadi Mutukula nchini Uganda.

“Zaidi ya shilingi bilioni 700 zimewekezwa ili kuwezesha sehemu ambayo sasa wananchi wanatumia saa mbili kuvuka kwa kutumia vivuko, daraja likikamilika, watatumia dakika nne”, amesisitiza Mhe. Silaa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi Balozi, Eng. Aisha Amour ameishukuru Kamati ya PIC kwa ushauri na miongozo kwa Wizara na kuihakikishia kuwa Wizara itasimamia kikamilifu ujenzi wa daraja hilo ili likamilke kwa wakati na ubora uliokusudiwa.

“Hatutamwongeza mkandarasi muda hivyo ajitahidi akamilishe kwa wakati na ubora kama mkataba unavyoelekeza”, amesisitiza Balozi, Eng. Aisha Amour .

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila amesema daraja hilo linalojengwa na kampuni ya M/s China Civil Engineering Construction Cooporation (CCECC), limetoa ajira zaidi ya elfu moja na asilimia 94.3 ya ajira hizo zikiwa za watanzania.

Daraja hilo lenye urefu wa KM 3 litakapokamilika litakuwa daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki na la sita kwa urefu barani Afrika.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)