Naibu Waziri wa Ardhi Geophrey Pinda akitoa onyo kwa Maofisa Ardhi Katavi wanaoshirikiana na Wenyeviti wa mitaa na vijiji kuuza maeneo au viwanja zaidi ya Mara moja.Picha na Mary Baiskeli.
Naibu Waziri wa Ardhi Geophrey Pinda akiwasili mjini Mpanda kwaajili ya ziara yake ya siku mbili kuzungumza na watumishi wa idara ya ardhi na NHC ili kuwakumbusha wajibu wao.Picha na Mary Baiskeli.
Naibu Waziri wa Ardhi Geophrey Pinda akizindua Baraza la Ardhi na Nyumba wilaya ya Mlele.Picha na Mary Baiskeli.
Baadhi ya viongozi wa halmashauri ya Mlele wakiwamo watumishi wa Baraza la Ardhi Mlele pamoja na wananchi.Picha na Mary Baiskeli.
Na MARY Baiskeli, Katavi.
Wenyeviti wa mitaa na vijiji Mkoani Katavi baadhi yao wametajwa kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi huku wakitupiwa lawama kushirikiana na Maafisa ardhi kuuza viwanja zaidi ya mara moja na wengine wanadaiwa kuuza hadi maeneo ya hifadhi.
Malalamiko hayo yanajili wakati wa ziara yake ya kikazi Naibu wa Ardhi Geophery Pinda baada ya kuwasili mkoani Katavi na kuzungumza na wadau na watumishi wa idara hiyo.
Wadau hao wametoa malalamiko hayo kwa Naibu Waziri wa Ardhi katika kikao kilichowakutanisha kwa pamoja wakiiomba serikali itafute njia mbadala ya kuwavua madaraka wenyeviti wanaokiuka maadili ya kazi.
Afisa Tarafa ya Kashauriri Manispaa ya Mpanda Mbonimpaye Nkoronko amesema migogoro mingi iliyopo ni ile ya viwanja kuuzwa kwa watu zaidi ya mmoja.
“Migogoro mingi inayokuja ofisi ya Mkuu wa wilaya chanzo kikubwa ni Wenyeviti wa mitaa na vijiji,tunakwenda kwenye vikao hakuna utaratibu wa kumuondoa kunakuwa na sintofahamu nyingi sana,”
“Wakati mwingine hawa wenyeviti wanashirikiana na maofisa ardhi hao hao,kuuza maeneo zaidi ya mara moja tunaomba hili liangaliwe Mhe. Naibu Waziri,”
Baada ya changamoto hiyo kuwasilishwa Naibu Waziri wa Ardhi Geophery Pinda akatoa kalipio kali kwa Maofisa Ardhi wanaojihusisha na tabia hiyo akiwataka kufanya kazi kwa uadilifu.
“Badala ya kwenda kuwakumbatia wasiokuwa na maslahi katika maisha yenu achene msiwakumbatie,tusimame kwenye ukweli ili tuoge,”
“Mimi nashangaa sana kila nikiangalia kwenye kitabu cha malalamiko hakuna linaloigusa wizara moja kwa moja,”
“Kwasababu walishafanya kazi ya kupima na kumaliza,wasimaizi wa maeneo yale ni madiwani na wengine ndo wanatuharibia, hivi Mwenyekiti wa mtaa anaweza kukuhonga shilingi ngapi?badilikeni tuwe imara,”amesema Pinda.
Ziara ya Pinda imekwenda sambamba na kuzindua baraza la ardhi na nyumba halmashauri ya Mlele ambalo ni mwarobaini wa kumaliza changamoto ya wakazi kwenda Mpanda kupata huduma.
Aidha amesisitiza Mabaraza ya ardhi mkoani Katavi kutofanya kazi kama mahakama, badala yake yatimize wajibu wake mithili ya machifu kujikita kutoa usuluhushi.
“Baadhi ya mabaraza yamekuwa ni chokochoko lakini siyo hapa Mlele sijasikia, kwakuwa ndiyo nimeingia kwenye familia hii nitafuatilia,”
“Mimi nawaamini sana tujitahidi kule kwenye mabaraza yetu siyo mahakama sisi ni badala ya machifu kupatanisha wakishindwa peleka taarifa kwa Mwenyekiti na nyie wananchi msilazimishe migogoro,”
Naye Mkuu wa wilaya ya Mpanda Majid Mwanga amesema hatasita kumfikisha Takukuru kiongozi yeyote wa baraza la ardhi atakaye kiuka utaratibu ikiwamo kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Awali akisoma taarifa kaimu Msajili wa mabaraza ya ardhi na nyumba kanda ya Magharibi Emmanuel Mwambigija amebainisha changamoto zinazowakabili ni uhaba wa vitendea kazi.
“Furniture zilizopo hazitoshelezi,kompumta na usafiri baraza la Mpanda na Mlele hakuna gari,huwa tunatembelea migogoro hivyo kuyafikia maeneo ili kutoa haki inakuwa changamoto,”
Naye Mkuu wa wilaya hiyo Majid Mwanga akatoa angalizo kwa viongozi wa baraza hilo endapo wakikiuka utaratibu watachukuliwa hatua.
“Sitegemei kuona hukumu yeyote imetolewa kwenye baraza la kata au kijiji nikisikia Takukuru itakuhusu leo hapa mmepata semina nawaomba sana mkafanye kazi ya usuluhishi,”
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Said Mbogo amesema uwepo wa baraza hilo utaondoa adha kwa wakazi kwenda Mpanda kupata huduma.
“Wananchi ilikuwa inawalazimu kutembea umbali mrefu zaidi ya kilometa 100 kwenda mpanda wengine walikosa haki kwakushindwa kumudu gharama,”
Baraza la Mlele tangu kuanzishwa kwake limepokea mashauri 25 kati yake 13 yamesikilizwa na kutolewa maamuzi zinazoendelea kusikilizwa ni 34.