MSINICHUKIE NINAPOSEMA MGANGA MKUU WA WILAYA AONDOLEWE - DKT. MOLLEL

MUUNGANO   MEDIA
0

 


NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka Wataalamu wa Afya kutomchukia pindi anapofanya maamuzi ya kumtoa Mganga Mkuu wa Wilaya kwani hufanya hivyo kwa nia njema ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi. 

Dkt. Mollel ametoa wito huo alipomwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu katika maadhimisho ya miaka 70 ya Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.

"Msinichukie saa zingine naposema ondoa DMO, unakuta DMO kwenye akaunti yake kuna milioni 390 alafu hakuna Dawa, alafu kuna milioni 10 zimetumika ukiuloza anakwambia nimenunua Dawa za idara ya meno, ukiuliza kiongozi wa Idara ya meno anakwambia hajawai kuona kitu, sasa huo lazima tuwatandike." Amesema Dkt. Mollel.

Sambamba na hilo Dkt. Mollel ametoa wito kwa Wataalamu kuunga mkono jitihada za Serikali za kuja na Sheria ya Bima ya afya kwa woteitayotoa fursa kwa wananchi kupata matibabu katika hospitali yoyote nchini kuanzia zahanati mpaka taifa.

Ameendelea kusisitiza kuwa, Bima ya Afya kwa wote itasaidia kupunguza misamaha ya matibabu ambapo fedha hizo zitaelekezwa kuboresha maslahi ya watoa huduma za afya katika vituo vyao.

Pia, amewataka Wataalamu wa afya hususan Wauguzi kufanya kazi kwa juhudi, kuwa waadilifu kwa kufuata miiko na vioapo vyao vya utoaji huduma ili kuitenda kazi yao kwa haki na kuondoa manung'uniko kutoka kwa wananchi.

Pamoja na hayo kwa niaba ya Waziri wa afya amewapongeza watoa huduma wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia wananchi licha ya changamoto wanazokutana nazo, huku akiweka wazi kuwa, Serikali itaendelea kuboresha maslahi yao.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)